Salaam za Mchungaji Kiongozi, Charles Mzinga

Bwana asifiwe washarika, ni fursa nyingine adimu ya kujikumbusha na kupeana taarifa juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea hapa usharikani kwetu Azaniafront na kanisa zima kwa ujumla.

Ikiwa tunamaliza robo ya kwanza ya mwaka 2020, shughuli mbalimbali zimeweza kufanyika hapa usharikani katika kipindi hiki cha miezi mitatu kama ambavyo utapata fursa ya kuzisoma kwa kina ndani ya toleo hili la Kijarida. Pia niwakumbushe washarika kutembelea tovuti rasmi ya usharika ambayo ni www.azaniafront.org ili kupata taarifa na matukio mbalimbali yanayohusu usharika wetu.

Ili kurahisisha mawasiliano baina yetu, kila kikundi hapa usharikani kina group la WhatsApp, niwaombe washarika wote muweze kutumia magroup hayo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kufikishiana taarifa muhimu zinazohusu usharika wetu. Hii itatusaidia kukaa tukiwa wamoja na rahisi kufamishana jambo kwa haraka pale inapobidi.

Pia, natoa pongezi za dhati kwa washarika wote kwa kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika utekelezaaji wa kazi na mipango mbalimbali ya usharika, lakini pia kwa kujitolea kusaidia jamii zinazokuwa na uhitaji kama watoto yatima, wazee pamoja na wagonjwa.

Kuhusu janga la Virusi vya Corona (COVID-19) linaloitesa dunia kwa sasa, niwaombe washarika kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia malekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo hatari. Taarifa kwa kina na hatua ambazo usharika umechukua katika kupambana na janga hili zinapatikana katika ukurasa wa pili wa kijarida hiki. Kama uongozi wa usharika, ni jukumu letu kuhakikisha afya za washarika wote zinakuwa katika hali ya usalama.

Tuendelee kumwomba na kumtumikia Mungu wetu ili atuepushe na majanga ya aina mbalimbali. Pia, tuendelee kujitolea kusaidia watu wengine wenye uhitaji pale inapobidi maana kwa kufanya hivyo tunamtukuza Bwana wetu aliye hai.

Mungu awabariki wote..!

 

Kwa taarifa zaidi kuhusu usharika, usikose kupata nakala ya Kijarida namba 8 cha Usharika wa Azaniafront toleo la Januari - Machi 2020.