Date: 
01-03-2023
Reading: 
Mathayo 4:1-12

Hii ni Kwaresma 

Jumatano asubuhi tarehe 01.03.2023

Mathayo 4:1-11

1 Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi.

2 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.

3 Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.

4 Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,

6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.

7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.

8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,

9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.

10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.

11 Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.

Tukimtegemea Bwana tutashinda majaribu;

Asubuhi ya leo katika somo tulilopewa tunamuona Yesu akijaribiwa kwa siku arobaini nyikani, ambapo "hakula kitu" lakini zilipotimia siku 40, aliona njaa.

Injili hii inatufundisha nini?

1.Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu.

Katika Injili ya Luka inaaandikwa kuwa Yesu alijaa Roho Mtakatifu;

Luka 4:1

[1]Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani,

Bila shaka Roho Mtakatifu ndiye aliyemuwezesha Yesu kushinda majaribu ya Ibilisi. Hapa tunalashwa kutafakari kama tunaongozwa na huyu Roho Mtakatifu.Kama Yesu mwenyewe aliongozwa na Roho Mtakatifu, sisi hatuwezi kuukwepa uongozi wa Roho Mtakatifu.

2. Kama Yesu mwenyewe alijaribiwa, sisi hatuwezi kukwepa majaribu.

Tafsiri yake; Maisha tunayoishi yana changamoto nyingi ambazo hazikwepeki. Lakini kama Yesu alivyoshinda, na sisi tunaweza kushinda.

Angalizo;

Tusiwe changamoto kwa wenzetu, yaani wewe usiwe kikwazo kwa mwenzako, bali tusaidiane, tuinuane, tuelimishane, lakini zaidi tupendane. 

Kumbuka;

Luka 17:1-2

[1]Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!

[2]Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa.

Tusisababishiane changamoto za maisha, zitakazoingiza wenzetu kwenye majaribu, bali tusaidiane kuondoka majaribuni, tukiuchukua mfano wa Yesu aliyeshinda majaribu.

3. Shetani analijua neno la Mungu.

Ibilisi alipomwambia Yesu ajitupe chini, alimpa neno pia, akinukuu maandiko;

Mathayo 4:6

[6]akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, 

Atakuagizia malaika zake; 

Na mikononi mwao watakuchukua; 

Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.

Unajua shetani alinukuu wapi?

Zaburi 91:11-12

[11]

Kwa kuwa atakuagizia malaika zake 

Wakulinde katika njia zako zote.

[12]Mikononi mwao watakuchukua, 

Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.

Hapa tunakumbushwa kuwa lazima tuwe na bidii ya kulijua neno la Mungu sana, ili tuweze kushinda majaribu. Tafuta muda wa kutosha kujifunza neno la Mungu nyumbani, ibadani, nyumba kwa nyumba, semina, kongamano, ili mradi neno la Mungu linafundishwa kwa usahihi wake.

4. Yesu alitumia neno la Mungu kushinda majaribu ya Ibilisi.

Katika somo tulilosoma, tuaona kuwa Yesu alipoambiwa na Ibilisi kufanya jambo fulani, alitumia neno la Mungu. mfano, alipoambiwa abadili jiwe kuwa mkate, alijibu kuwa mtu hataishi kwa mkate tu

Mathayo 4:3-4

[3]Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.

[4]Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

Yesu alitumia andiko hili;

Kumbukumbu la Torati 8:3

[3]Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana.

Pia shetani alipomwambia Yesu ajitupe chini, Yesu alimjibu akisema usimjaribu Bwana Mungu wako. Yesu anatumia andiko hili;

Kumbukumbu la Torati 6:16

[16]Msimjaribu BWANA, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa.

Hapa tunajifunza kuwa neno la Mungu ndilo suluhisho la mambo mambo yote. Tuwe na utamaduni wa kusoma, kutafakari, na kuliishi neno la Mungu ndipo tutashinda majaribu.

5. Tusiitii sauti ya mwovu shetani.

Yesu alipoambiwa abadili jiwe kuwa mkate alikuwa hashindwi! Kumbuka ni Yesu huyu huyu aliyebadili maji kuwa divai, ni Yesu huyu aliyetembea juu ya maji, alimfufua Lazaro na kijana wa Naini, ni Yesu huyu aliyelisha waume elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, ndiye aliyemponya kipofu Bartmayo n.k

Yesu hakubadili jiwe kuwa mkate, mojawapo ya sababu ikiwa ni kutotii sauti ya mwovu shetani.

Sisi leo tunahimizwa kutoitii sauti ya mwovu shetani. Tunaitii sauti ya shetani tunapotenda dhambi. Tunaweza kutoitii sauti ya shetani tukimtegemea Mungu peke yake.

Dhambi ni ibada

Unapotenda dhambi unakuwa ibadani ukimwabudu shetani. Mtegemee Yesu ili kushinde shetani.

Namaliza kwa kukueleza yafuatayo;

i. Kujiona tuko imara kiasi kwamba hatuwezi kuingia dhambini kunatufanya tuwe na mazingira magumu. Hii ni kwa sababu sisi hatuna nguvu ya kushinda dhambi. Mungu ndiye anayetuwezesha kushinda dhambi. Tunakuwa na mazingira magumu kwa sababu tunatumia akili zetu na uwezo dhaifu kuikabili dhambi.

ii. Hakuna jaribu linalotujia ambalo halijawahi kuwa sehemu ya mwanadamu. Hatujaribiwi na jambo jipya, au lisilo la kawaida.

iii. Mungu ni mwaminifu, hataruhusu jaribu linalotuzidi kutujia. Atatuwekea njia ya kushinda.

Tuwe wavumilivu tukimlilia Mungu katika majaribu tunayopitia, kwa kuwa Mungu wetu ni mwaminifu, na ameahidi kutotuacha tujaribiwe kupita uwezo wetu

Siku njema.

Heri Buberwa