Date: 
12-01-2022
Reading: 
Matendo 8:9-13

Jumatano asubuhi tarehe 12.01.2022

Matendo ya Mitume 8:9-13

9 Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa.

10 Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.

11 Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake.

12 Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.

13 Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.

Wabatizwao ndio wana wa Mungu;

Filipo anahubiri katika Samaria, mji ambao ulikuwa na watu wasioamini. Mji huo ulikuwa na mchawi mmoja aitwaye Simoni, huyu alionekana mtu mkubwa sababu ya uchawi. Wengi waliacha imani za uchawi, wakabatizwa wakimpokea Yesu kwa Injili aliyohubiri Filipo. Simoni naye alibatizwa! Akashangaa ishara zilizotendeka akiwa na Filipo.

Baada ya kubatizwa, watu wa Samaria walikuwa wana wa Mungu. Ni kama sisi leo, ambavyo tukibatizwa tunakuwa wana wa Mungu. 

Baada ya kubatizwa pia, waliziona ishara hadi wakastaajabu. Ipo neema ya ubatizo katika Yesu Kristo, pale tunapompokea na kumfanya awe kiongozi wetu. Tuyashuhudiayo ni tofauti na wasioamini, maana sisi twaiona neema ya Kristo kuelekea uzima wa milele.

Tumuige Filipo, aliyehubiri watu wakabatizwa. Ni muhimu kuendelea kuwaleta watu kwa Yesu. Tusiifurahie neema hii peke yetu. Mungu anataka watu wote wamwendee na kuwa wake. Hivyo ni jukumu letu kuwaleta watu kwake wabatizwe, na utukufu wake upate kudhihirika kwa wote.

Uwe na mapumziko mema.