Date: 
14-03-2022
Reading: 
Matendo 17:5-9

Hii ni Kwaresma 

Jumatatu asubuhi tarehe 14.03.2022

Matendo ya Mitume 17:5-9

5 Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji;

6 na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako,

7 na Yasoni amewakaribisha; na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema na kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu.

8 Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo.

9 Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao.

Tupinge ukatili;

Mitume wakiwa wanaendelea na kazi yao, wanafika Thesalonike na kuhubiri habari za Yesu aliyekufa na kufufuka kwa ajili ya ulimwengu wote. Wapo walipoamini na kuungana na akina Paulo na Sila.

Wapo Wayahudi waliochukia kazi ya Mitume, hadi kufanya ghasia mjini. Mtu aitwaye Yasoni aliwakaribisha baadhi ya Mitume nyumbani kwake. Huyu alivamiwa na Wayahudi, kwa lengo la kufanya fujo na kuwashtaki Mitume husika, kwa sababu tu walihubiri kuhusu Yesu.

Wayahudi wanawazuia Mitume kufanya kazi yao. Wanawashambulia mitume na kuwashtaki mbele ya wakubwa wa mji kwa sababu ya Injili waliyoihubiri. Kwani Mitume kuhubiri walikuwa na kosa gani? Hadi kuwashambulia, kuwashikilia na kuwashtaki? Kwanza walivuruga ratiba ya mitume, pili waliwazuia kufanya kazi yao, tatu wanazuia neno la Mungu lisienee kwa wengi. Huu ni uovu! Ni ukatili!

Tafakari mambo unayofanya kama yanazuia kazi za wengine. Tafakari kama kazi zako zinawapa au kuwanyima wengine haki na uhuru wao. Tunaalikwa kutenda yatupasayo, tukiwapa watu haki zao, bila kuwasumbua, ili wafikie malengo yao katika kumtumikia Mungu.

Nakutakia juma jema lisilo na ukatili.