Date: 
14-10-2021
Reading: 
Isaya 50:4-9

ALHAMISI TAREHE 14 OKTOBA 2021, ASUBUHI.

Isaya 50:4-9

4 Bwana MUNGU amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao.

5 Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma.

6 Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate.

7 Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.

8 Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi.

9 Tazama, Bwana MUNGU atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa? Tazama hao wote watachakaa kama vazi; nondo atawala.

Nguvu ya imani katika Yesu Kristo;

Nabii Isaya anaandika akionesha jinsi ambavyo Mungu anaweza kumuaibisha au kumthibitisha mtumishi wake. Anaonesha kuwa BWANA anawataka watu wafundishwao, wasio wakaidi. BWANA ndiye ampatiaye haki mtumishi wake na kumsaidia.

Bila shaka Isaya anaadika juu ya mtu anayemcha BWANA, mtumishi wake. Huyu ndiye awezaye kuthibitishwa na BWANA.

Sasa kuna uchaguzi hapa;

Unataka kuthibitishwa au kuaibishwa na BWANA? Kwa vyovyote jibu ni kuwa sote tunataka kuthibitishwa na BWANA wetu. Basi tuwe watu wafundishwao, tusio wakaidi, ndipo BWANA atatusaidia na kutupa haki ya uzima. Tutaweza kuthibitishwa na BWANA tukiwa na imani katika Yesu Kristo.

Nakutakia mapumziko mema.