Date: 
07-10-2021
Reading: 
Ezekiel 20:17-26

Alhamisi asubuhi; 07.10.2021

Ezekieli 20:17-26

[17]Walakini jicho langu likawahurumia nisiwaangamize kabisa, wala sikuwakomesha kabisa jangwani.

[18]Kisha nikawaambia watoto wao jangwani, Msiende katika amri za baba zenu, wala msizishike hukumu zao, wala msijitie unajisi kwa vinyago vyao.

[19]Mimi ni BWANA, Mungu wenu; endeni katika amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzitenda;

[20]zitakaseni sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

[21]Lakini watoto hao waliniasi; hawakuenda katika amri zangu, wala hawakuzishika hukumu zangu kuzitenda, ambazo mwanadamu ataishi kwazo kama akizitenda; walizitia unajisi sabato zangu, ndipo nikasema, kwamba nitamwaga ghadhabu yangu juu yao, ili kuitimiza hasira yangu juu yao jangwani.

[22]Lakini naliuzuia mkono wangu, nikatenda kwa ajili ya jina langu, lisitiwe unajisi mbele ya macho ya mataifa, ambao mbele ya macho yao naliwatoa.

[23]Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali;

[24]kwa sababu hawakuzitekeleza hukumu zangu, bali walizikataa amri zangu, nao walizitia unajisi sabato zangu, na macho yao yaliandama vinyago vya baba zao.

[25]Tena naliwapa amri zisizokuwa njema, na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo;

[26]nami nikawatia unajisi kwa matoleo yao wenyewe, kwa kuwa walipitisha motoni wote waliofungua tumbo; ili kuwafanya kuwa ukiwa, wakapate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

Tuwapende na kuwajali watoto;

Mungu alisikitika sana Israeli kuendela kumuasi, lakini aliendelea kujawa na huruma bila kuwaangamiza, akiwaambia kuzishika amri zake. Cha ajabu, hata watoto walimuasi Mungu! (21)

Watoto huwa hawawezi kufanya maamuzi peke yao. Kama walimuasi Mungu kama tulivyosoma, bila shaka waliongozwa na wazazi wao. 

Tujiulize;

Sisi tunawalea watoto katika njia sahii, au tunawaongoza kumuasi Mungu? Na tunapowaongoza kumuasi Mungu tunajenga jamii ya aina gani? Tunajenga Kanisa la aina gani? Tunaitwa kuzishika amri za Mungu, tukiwafundisha watoto wetu kuzishika pia, ili kujenga jamii inayomcha BWANA kwa pamoja kama Taifa lake.

Siku njema.

Heri Buberwa