Date: 
17-01-2022
Reading: 
1Wafalme 17:17-24

Jumatatu asubuhi tarehe 17.01.2022

1 Wafalme 17:17-24

17 Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena.

18 Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu?

19 Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake.

20 Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe.

21 Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena.

22 Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka.

23 Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai.

24 Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la Bwana kinywani mwako ni kweli.

Mungu hutakasa nyumba zetu;

Nabii Eliya alitumwa na Bwana kwenda mji wa Sarepta (9) Bwana akimwambia atamkuta mama mjane wa kumtumza. Alipofika huko, mwanamke mjane akamwambia kuwa alikuwa na kiasi kidogo tu cha unga, atengeneze mkate ale na mwanae, wale wafe, maana chakula kingeisha. Eliya akamwambia kwanza amtengenezee yeye mkate. Pipa lake la unga na chapa ya mafuta havikupunguka tena.

Baada ya hapo, ndipo katika somo la leo tunaona mtoto katika nyumba ile akifa. Mama anamwendea Eliya akilalamika na kumuuliza kuwa alikuja pale nyumbani ili dhambi yake ikumbukwe na mtoto wake afe? Eliya anamwomba Bwana, na mtoto anafufuka.

Huyu mama mjane wa Sarepta alipata chakula katikati ya njaa kali. Mtoto wake alifufuka toka kifoni, akafufuka kwa msaada wa Bwana. Kwa baraka hizi, ni dhahiri Mungu alitakasa nyumba ya mama huyu mjane.

Mungu alitakasa nyumba ya mama mjane huyu wa Sarepta kwa kuwa alimkaribisha Eliya, mtumishi wa Bwana. 

Nasi tukimkaribisha Yesu anatakasa nyumba zetu na kutubariki.

Nakutakia wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio.