Date: 
13-02-2023
Reading: 
Yeremia 31:10-14

Jumatatu asubuhi tarehe 13.02.2023

Yeremia 31:10-14

10 Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali; mkaseme, Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.

11 Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.

12 Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, wataukimbilia wema wa Bwana, nafaka, na divai, na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng'ombe; na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji; wala hawatahuzunika tena kabisa.

13 Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, na vijana na wazee pamoja; maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.

14 Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono, na watu wangu watashiba kwa wema wangu, asema Bwana

Neno la Mungu lina nguvu;

Bwana Asifiwe;

Nabii Yeremia analiita Taifa la Mungu kulisikia neno la Bwana katika maisha yao. Yeremia anawaita watu wa Mungu wasiishie kulishika tu neno la Mungu, bali wawatangazie wengine neno la Mungu. Anaendelea kuonesha kuwa kwa mamlaka ya neno lake, Mungu aliwakomboa Israeli kutoka utumwani. Somo linaonesha watu kufurahia maisha yao kwa sababu ya kusikia neno la Mungu.

Ujumbe wa Nabii Yeremia asubuhi ya leo ni kwa kundi la waaminio, yaani Kanisa kulisikia neno la Mungu. Neno la Mungu linayo nguvu ya kutuongoza katika njia sahihi. Tusikilize mahubiri, tusome Biblia, tukiomba msaada wa Roho Mtakatifu kuelewa tusomayo na kusikiliza. Tukilielewa neno la Mungu na kulishika tunakuwa katika njia sahihi ya kuurithi uzima wa milele. 

Uwe na wiki njema yenye ushuhuda.

Heri Buberwa