Date: 
26-09-2025
Reading: 
Marko 12:41-44

Ijumaa asubuhi tarehe 26.09.2025

Marko 12:41-44

41 Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.

42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.

43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;

44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.

Tunaitwa kuwa mawakili wa Mungu;

Yesu alikuwa hekaluni, ulipofika muda wa matoleo akawa anaangalia watu walivyokuwa wanaweka matoleo yao kwenye sanduku. Matajiri waliweka hela nyingi lakini alikuwepo mwanamke mjane, na maskini aliyeweka senti mbili! Yesu akawaambia wanafunzi wake kwamba huyu mjane aliweka zaidi kuliko wengine walioweka mali iliyowazidi, maana kwa umaskini wake alitoa vyote alivyokuwa navyo.

Somo hili huwa halimaanishi kuchukua mali yako yote ukaitoa sadaka, bali kumtolea Mungu kwa moyo. Unaweza kutoa mali yote ukaishia kuwa karibu na Kanisa, mbali na Mungu. Tukitoa kwa moyo tutatoa inavyostahili. Tukiitambua neema ya wokovu kwetu hatutatoa mali inayotuzidi, bali tutamtolea Bwana kadri anavyotujalia tukijua kwamba sisi ni mawakili wake. Amina

Ijumaa njema

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com