Date: 
02-09-2025
Reading: 
1 Samweli 17:8-11

Jumanne asubuhi tarehe 02.09.2025

1 Samweli 17:8-11

8 Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi.

9 Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia.

10 Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane.

11 Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.

Mungu huwapinga wenye kiburi;

Zamani za kale alikuwepo mtu mmoja Goliati. Huyu alikuwa anatisha, maana alikuwa shujaa katika kambi ya Wafilisti. Alitokea upande wa Wafilisti, akawataka Israeli wateue mmoja kati yao, ambaye angepigana na huyo Goliati. Kama Goliati angeshinda, basi Israeli wangewatumikia Wafilisti. Na kama Goliati angeshindwa, basi Wafilisti wangewatumikia Israeli.

Israeli waliogopa sana wakawa hawana la kufanya zaidi ya kurudi nyuma. Daudi kwa ujasiri mkubwa alikiri kumkabili Goliati kwa jina la Bwana wa majeshi. Huku Goliati akitisha kama kawaida yake, Daudi alimuua kwa jiwe aliloliweka kwenye kombeo. Goliati akafa! Wafilisti wakakimbia! Goliati alikuwa na kiburi, lakini Daudi alimshinda Goliati kwa jina la Bwana. Kiburi hakina faida, acha!

Siku njema.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com