Jumamosi asubuhi tarehe 26.07.2025
1 Mambo ya Nyakati 28:8-10
8 Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la Bwana, na masikioni pa Mungu wetu, angalieni na kuzitafuta amri zote za Bwana, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele.
9 Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa Bwana hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele.
10 Jihadhari basi; kwani Bwana amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.
Tudumu katika fundisho la Kristo;
Mfalme Daudi aliwakusanya watu wote katika Yerusalemu, akaanza kuwahutubia jinsi alivyokuwa amepanga kujenga nyumba kwa ajili ya kustarehe kwa sanduku la Agano la Bwana. Daudi anaendelea kusema kuwa Bwana alimwambia kwamba asingejenga nyumba hiyo kwa sababu alikuwa mtu wa vita na alikuwa amemwaga damu. Badala yake Daudi anasema Bwana alikuwa amemteua Suleimani kujenga hekalu, akiwa na ufalme ulio imara.
Somo la asubuhi hii ni hotuba ya Daudi ikiendelea, ambapo Daudi anahutubia umati na kumwambia Suleimani kuwa amjue Mungu akamtumikie kwa moyo mkamilifu, maana Bwana amemchagua kuijenga nyumba takatifu ya Bwana. Suleimani aliitwa na kuchaguliwa kujenga nyumba ya Bwana ili Bwana aendelee kuabudiwa. Vivyo hivyo nasi tumechaguliwa na Bwana ili tumwamini na kumtumikia. Basi tudumu katika fundisho lake ili tuurithi uzima wa milele. Amina
Jumamosi njema
Heri Buberwa