Date: 
19-05-2025
Reading: 
Zaburi 68:24-27

Hii ni Pasaka

Jumatatu asubuhi tarehe 19.05.2025

Zaburi 68:24-27

24 Ee Mungu, wameiona miendo yako; Miendo ya Mungu wangu, Mfalme wangu, katika patakatifu

25 Waimbaji hutangulia, nyuma yao wapigao vinanda, Kati ya wanawali wapiga matari.

26 Mhimidini Mungu katika mikutano, Bwana katika makusanyiko ya Israeli.

27 Yuko Benyamini mdogo, mtawala wao; Wakuu wa Yuda, kundi lao; Wakuu wa Zabuloni; Wakuu wa Naftali.

Kila mwenye pumzi amsifu Bwana;

Zaburi ya 68 ni Zaburi ya Daudi inayomuongelea Mungu kwa lugha ya kijeshi. Daudi anaimba kuhusu Mungu kama kiongozi mshindi wa kijeshi aliye juu ya Sayuni. Zaburi imegawanyika katika mtiririko wa sehemu saba ambapo Bwana anaonekana kushinda na kuchukua nafasi kama Mfalme wa Sayuni. 

Mgawanyiko wa Zaburi hii uko kama ifuatavyo;

1. Mungu anawatawanya adui (1-3)

2. Mungu mwenye haki, Mfalme mwema (4-6)

3. Mungu mtoaji, mwenye baraka (7-10)

4. Mungu mshindi (11-14)

5. Mungu katika Sayuni (15-18)

6. Mungu wa wokovu na kifo (19-23)

7. Sifa na Utukufu kwa Mungu (24-35)

Sehemu ya saba ndiyo ina ujumbe wa asubuhi ya leo, yaani Sifa na Utukufu kwa Mungu. Sifa toka kwa watu wote zinaelekezwa kwa Mungu. Kila mmoja toka makabila yote anaelekezwa kumsifu Mungu. Mstari wa 28 hadi 31 unahusu watawala wa mataifa kuingia hekaluni na kumsifu Mungu. Ufalme wa Mungu ulikuwepo, na watawala wote katika Israeli walielekezwa kumsifu Mungu Mfalme aliye juu ya vyote. Hitimisho la Zaburi linakuwa ni watu wote kumsifu Mungu.

Wayahudi walisoma maandiko kwa kuiangalia jamii yao. Yaani kama Zaburi ingeongelea ushindi, waliangalia ushindi wao, na kwa sababu walimtazamia Mesiya, walihusianisha ushindi na Mesiya ajaye kuwakomboa. Njia hii ya kutafsiri maandiko inaonekana kwenye Agano jipya ambapo waandishi walitafsiri Agano la kale kulingana na siku zao na Mesiya mfano;

Marko 7:6

Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali nami;

Hapa Isaya hakuwa hakuwa anatabiri kwa watu wa miaka ya 30BK, lakini kwa watu wake aliokuwa nao 740KK. Lakini Zaburi na manabii walieleweka katika ujumbe endelevu, na Yesu aliutumia ujumbe wa manabii katika siku alizohubiri, utamaduni uliokuwa wa Kiyahudi. 

Mtume Paulo ananukuu sehemu ya Zaburi ya 68;

Waefeso 4:7-8

7 Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.
8 Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa.

-Sasa kwa maana hiyo, hatuwezi kurudi Zaburi ya 68 na kusema Zaburi inamhusu Daudi na Mesiya, haituhusu leo. Ni ushindi wa Mesiya mtarajiwa katika Zaburi ya 68, waliyetarajia awaondolee utawala wa Kirumi. Lakini kwa kunukuu Zaburi ya 68, Paulo anamtaja Yesu Kristo kama Mfalme akaaye kwenye kiti cha enzi, atawalaye mataifa, astahiliye kusifiwa. Ndipo tunapata ujumbe wa moja kwa moja kumsifu Mungu aliye Mfalme wetu. Sifa zetu kwake ziwe zaidi ya kuimba, yaani maisha yenye ushuhuda. Amina

Uwe na wiki njema

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com