Event Date: 
17-04-2025

Katika ibada ya Alhamisi Kuu iliyofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral, 17 Aprili 2025 na kuongozwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Baba Askofu Dkt. Alex Malasusa iliwakutanisha washarika na wageni mbalimbali kukumbuka siku ambayo mwokozi wetu Yesu Kristo alisalitiwa na mmoja wa wanafunzi wake aliyejulikana kama Yuda Iskarioti na hivyo kupelekea kukamatwa, kuteswa msalabani mpaka kufa kwake. 

Somo: Agano Jipya Katika Damu ya Yesu ~ Luka 22: 14 - 20

Akihubiri katika ibada hiyo iliyoambatana na Kushiriki Meza ya Bwana, Msaidizi wa Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Chediel Lwiza aliwakumbusha washarika umuhimu na namna ya kushiriki Chakula Kitakatifu. Dean Lwiza alikumbusha namna ambavyo Yesu Kristo alivyowaambia wanafunzi wake kabla ya kushiriki Chakula cha Bwana kuwa mmoja wa wanafunzi wake atamsaliti jambo lililoleta mshutuko mkubwa miongoni mwa wanafunzi wake na wakaanza kujihoji ni nani miongoni mwao alikuwa na mpango huo (Yohana 13: 23-27). 

"Yesu anatukumbusha uhusiano wetu na Mungu, Uhusiano wetu na Yeye na Chakula Kitakatifu ambacho hakiliwi pasipo kukiandaa vizuri, pasipo kujihoji vizuri, tena sio kujihoji kwa kawaida, bali kujihoji na kuona uchungu ndani. Tunapokuja kushiriki Meza ya Bwana lazima tujihoji," alisema Dean Lwiza.

"Mungu anapotupa neema hii, kipindi hiki cha kupata Chakula Kitakatifu cha Bwana, tusije tukashiriki hiki chakula kama tunakula mkate wa mabumunda, huu sio mkate wa mabumunda wala ugali wa dona, wala sembe, sio kiti moto hiki...., hapana. Ni Chakula cha Yesu na kina madai makubwa ya kiroho." aliongeza Dean Lwiza.

Baadhi ya Matukio katika Picha kutoka kwenye ibada za Alhamisi Kuu (Tazama hapa chini).

Tazama Ibada zote za Alhamisi Kuu hapa:

1. Ibada ya Kiingereza (English service): https://www.youtube.com/watch?v=RD-telAQFyg

2. Ibada ya Kiswahili (Swahili Service):  https://www.youtube.com/watch?v=mq-MpL-bQgI

---------#####---------