Hii ni Kwaresma
Jumanne asubuhi tarehe 08.04.2025
Mambo ya Walawi 16:11-19
11 Na Haruni atamsongeza ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake; naye atamchinja yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake.
12 Kisha atatwaa chetezo kilichojaa makaa ya moto yatokayo katika madhabahu iliyo mbele za Bwana, na konzi mbili za uvumba mzuri uliopondwa sana, mikononi mwake, naye atauleta ndani ya pazia.
13 Kisha atatia ule uvumba juu ya moto mbele za Bwana, ili moshi wa ule uvumba ukisitiri kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, asije akafa.
14 Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba.
15 Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya vile vile kama alivyofanya kwa damu ya ng'ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema,
16 naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao.
17 Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli.
18 Kisha atatoka na kuiendea madhabahu iliyo mbele za Bwana na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na ya damu ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote.
19 Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke.
Yesu ni Mpatanishi;
Baada ya watoto wawili wa Haruni kufa, Bwana anamwambia Musa, kuwa Haruni asikaribie mbele za Bwana, asije akafa. Bwana anamuelekeza Musa, jinsi ambavyo ataenda mbele za Bwana na sadaka kwa ajili ya upatanisho.
Kikubwa hapa, sikusudii kurejea historia ilikuwaje watoto wa Haruni wakafa, na ilikuwaje itolewe sadaka ya kuteketezwa. Kikubwa cha kurejea hapa ni kuwa kwa wakati ule, upatanisho ulifanyika kwa njia ya sadaka ya kuteketezwa.
Lakini kwa enzi hizi za Agano jipya, Yesu ndiye aliyejitoa kuwa sadaka kwa ajili yetu.
1 Petro 1:18-19
[18]Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; [19]bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.Hivyo hatuhitaji kuchinja mbuzi, Kondoo au mnyama yeyote, tumekombolewa kwa damu ya Yesu. Ujiulize; Ni kweli umekombolewa?
Maisha yako yanashuhudia kuwa umekombolewa na Yesu? chukua hatua ya Imani.
Yesu anakungojea.
Heri BuberwaNteboya.