Date: 
07-04-2025
Reading: 
Waebrania 5:1-5

Hii ni Kwaresma 

Jumatatu asubuhi tarehe 07.04.2025

Waebrania 5:1-5

1 Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi;

2 awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu;

3 na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi.

4 Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni.

5 Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.

Yesu ni Mpatanishi;

Tunalianza juma lingine kwa kumsoma Yesu kama Kuhani Mkuu. Yeye ndiye Kuhani Mkuu aliyewekwa kwa ajili ya wanadamu, akawa dhabihu kwa ajili ya wokovu. Kwa njia ya kifo chake, dhambi haina nafasi tena, maana yeye aliishinda dhambi. Kwa maana hiyo, dhambi haina nafasi ya kumuangamiza aaminiye, maana toba huondoa dhambi kwa msamaha utokao kwa Kristo mwenyewe.

Ukuhani Mkuu wa Yesu unaonekana kwa yeye kufanyika Mwokozi wa ulimwengu. Ukisoma mbele kidogo unauona mkazo wa ukuhani mkuu wa Yesu Kristo;

Waebrania 5:6

kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani wa milele Kwa mfano wa Melkizedeki. 

Majira haya yanatukumbusha kuwa Yesu Kristo ndiye Mwokozi wetu, aliyetuokoa kwa njia ya kifo msalabani. Ametupatanisha na Mungu kwa kutuokoa na dhambi, mwamini sasa uokolewe. Amina

Uwe na wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio. 

Heri Buberwa