Hii ni Epifania
Jumatatu asubuhi tarehe 03.02.2025
Mwanzo 9:8-17
[8]Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema,
[9]Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu;
[10]tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi.
[11]Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi.
[12]Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele;
[13]Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi.
[14]Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni,
[15]nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.
[16]Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi.
[17]Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi.
Mungu ni mlinzi wetu;
Tunaendelea na majira haya ya Ufunuo, ambapo leo asubuhi tunakumbushwa kuwa Mungu ndiye mlinzi wetu. Ni tafakari inayozidi kukazia kuwa, Mungu wetu ni wa Neema, yaani kwa Neema yake anatulinda. Wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi, watu walianza kuwa waovu machoni pa Bwana. Ndipo Mungu akasema,
Mwanzo 6:3
[3]BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.Wanadamu walikuwa waovu sana, hadi Mungu akaona kila kusudi la mwanadamu lilikuwa baya siku zote. Mungu alighairi na kuhuzunika, akaamua kumfutilia mbali mwanadamu aliyemuumba. Ni Nuhu tu aliyepata Neema machoni pa Bwana. Bwana alimwambia Nuhu atengeneze safina, aingie yeye na familia yake, na wanyama kama alivyomwelekeza. Mungu alileta gharika, na mvua ilinyesha kwa muda wa siku arobaini. Kila kitu kiliangamia na milima mirefu ilifunikwa. Yaani kila kitu kilichokuwa kwenye uso wa dunia kilifutiliwa mbali, na maji yalipata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini. Baadae maji yalikauka, na Nuhu akatoka kwenye safina, yeye na wanawe, na wanyama wote.
Sasa basi;
Ndipo katika Somo la Leo asubuhi, Mungu anaweka agano na Nuhu, akihaidi kutoangamiza tena kila kilichoko juu ya uso wa nchi kwa gharika. Hadi hapa tunakumbushwa kuwa;
1.Tutambue kuwa Mungu pekee ndiye anayetulinda.
Mungu ndiye alimlinda na kumkinga Nuhu na gharika.
Alimponya Nuhu na familia yake.
Nuhu alikufa akiwa na miaka mia tisa na hamsini, ambayo alipewa kuishi na Bwana.
Wewe unalindwa na nani?
2.Ahadi za Mungu ni timilifu.
Mungu anahaidi kuwa hataangamiza tena kwa gharika.
Ni kweli, haijatokea gharika tena!.
Kama Mungu alivyoahidi kutoleta gharika tena, Leo anatukumbusha kuwa yeye ndiye mlinzi wetu, ahadi ambayo ameitimiza kwa ukamilifu siku zote. Maana yake nini? Tuendelee kumwanini yeye aliyeahidi kuwa nasi siku zote.
Zaburi 121:7-8
[7]BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. [8]BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.3.Tuishi kwa kutenda mema.
Mungu alichagua Nuhu abaki baada ya gharika kwa kuwa alikuwa mchaji. Inatufundisha kuwa Mungu anapendezwa na watendao mema.
Baada ya Nuhu kupona na gharika, Mungu anahaidi kumlinda milele.
Sisi Leo, pamoja na kuwa Mungu amehaidi kutoleta gharika, tusiishi kwa kutenda maovu ambayo ni machukizo kwa Bwana, ili tuendelee kuifaidi Neema yake, ambayo ni ulinzi wake kwetu. Unaikumbuka baraka ya Bwana?
Ambayo iliamriwa na Mungu, kwa Musa kunena na Haruni, kwamba ndio mbaraka kwa wa Israel?
Hesabu 6:24-26
[24]BWANA akubarikie, na kukulinda;[25]BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili;
[26]BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani.Baraka hii huwa inatolewa na kiongozi wa ibada mwishoni mwa ibada, pamoja na kutupa baraka ya Bwana, lakini inatukumbusha kuwa Mungu ndiye anayetulinda.
Tudumu katika Imani ya kweli, katika ulinzi wa Bwana, ili Utukufu wa Mungu uzidi kuonekana. Amina.
Tunakutakia wiki njema
Heri Buberwa Nteboya