Alhamisi asubuhi tarehe 28.11.2024
Ufunuo wa Yohana 10:1-11
1 Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.
2 Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wa kushoto juu ya nchi.
3 Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao.
4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike.
5 Na yule malaika niliyemwona, akisimama juu ya bahari na juu ya nchi, akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni,
6 akaapa kwa yeye aliye hai hata milele na milele, yeye aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na nchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na wakati baada ya haya;
7 isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.
8 Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi.
9 Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.
10 Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.
11 Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.
Baada ya maisha haya, uzima wa milele;
Yohana anafunuliwa kuona malaika mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Malaika huyu ana kitabu kidogo kimefunguliwa. Malaika baada ya kulia kwa sauti kuu anasimama na kuinua mikono yake kuelekea mbinguni. Yohana anaelekezwa kula kitabu cha malaika na tumbo kutiwa uchungu, anaendelea kutoa unabii.
Malaika anayeonekana na Yohana, anaonesha nafasi ya Mungu aliye mkuu. Malaika alishuka kutoka juu mbinguni, halafu akanyoosha mikono kuelekea juu mbinguni.
Hii inatuonesha kwamba Mungu ndiye muumbaji wa mbingu na nchi, ambaye tukiamini na kufuata neno lake atatupa uzima wa milele. Amina
Alhamisi njema
Heri Buberwa