Jumanne asubuhi tarehe 19.11.2024
Ezekieli 17:22-24
22 Bwana MUNGU asema hivi; Mimi nami nitakitwaa kilele kirefu cha mwerezi, na kukipandikiza mahali; na katika vitawi vyake vilivyo juu nitatwaa kitawi kimoja kilicho chororo, nami nitakipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana;
23 juu ya mlima wa mahali palipoinuka pa Israeli nitakipanda; nacho kitatoa matawi, na kuzaa matunda, nao utakuwa mwerezi mzuri; na chini yake watakaa ndege wa kila namna ya mbawa; katika uvuli wa matawi yake watakaa.
24 Na miti yote ya mashamba itajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeushusha chini mti mrefu, na kuuinua mti mfupi, na kuukausha mti mbichi, na kuusitawisha mti mkavu; mimi, Bwana, nimenena, nami nimelitenda jambo hili.
Jiandae kwa hukumu ya mwisho;
Bwana anaikumbusha Israeli kuutambua ukuu wake. Toka pande zote za nchi, Bwana anasema kutwaa kila kitu, na nchi yote kuwa chini yake. Bwana anakumbusha kuwa katika nchi yote hakuna awezaye kuwa juu ya kitu chochote, ila yeye tu.
Katika mstari wa 24, Bwana anaonyesha Maajabu kwa kufanya anachotaka, mfano; kuushusha chini mti mrefu, na kuuinua mfupi,kuukausha mbichi na kuustawisha mkavu. Hapa Bwana anatoa picha kuwa yeye ndiye mwenye uweza. Yaani anaweza kufanya lolote, hata yale tunayodhani hayawezekani!
Bwana anadhihirisha ukuu wake katika dunia hii. Ni muhimu kulitambua hili, kwamba Utukufu wake hauna ubia!
Yeye aliyeumba ulimwengu, ndiye anayetawala, na ndiye atarudi kulichukua Kanisa. Kazi yetu ni kuamini na kutenda yatupasayo tukiendelea kumngojea.
Jiandae kwa hukumu ya mwisho.
Heri Buberwa