Date:
28-10-2024
Reading:
Warumi 3:27-31
Jumatatu asubuhi tarehe 28.10.2024
Warumi 3:27-31
27 Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani.
28 Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.
29 Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia;
30 kama kwa kweli Mungu ni mmoja, atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo.
31 Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.
Mwenye haki ataishi kwa imani;
Paulo anaendelea kuandika juu ya kuokolewa kwa Imani. Anasema hakuna kujisifu kwa aina yoyote wala sheria ya matendo, bali sheria ya imani. Paulo anakazia kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani, siyo kwa matendo ya sheria. Wapo Wayahudi ambao walifikiri Mungu ni wa kwao tu, lakini Paulo anasema Mungu ni wa wote, hivyo imani ni kwa wote.
Wokovu wetu hauna masharti, kwamba fanya hivi, Mungu afanye hivi. Huo ni utapeli. Wokovu ni kwa neema tu, kwa njia ya Yesu Kristo. Tunaokolewa kwa neema, kwa njia ya imani. Tunakuwa wenye haki mbele za Mungu kwa njia ya imani tu. Tengeneza maisha yako kwa kumwamini Yesu tu. Amina
Tunakutakia wiki njema yenye Matengenezo maishani.
Heri Buberwa