Date: 
27-07-2024
Reading: 
Zaburi 34:19-22

Jumamosi asubuhi tarehe 27.07.2024

Zaburi 34:19-22

19 Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.

20 Huihifadhi mifupa yake yote, Haukuvunjika hata mmoja.

21 Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.

22 Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.

Neema ya Kristo yatuwezesha;

Zaburi tunayosoma asubuhi ya leo inaonesha kuwa Bwana humponya na mateso mtu mwenye haki. Humtunza na kumlinda. Zaburi inaendelea kusema kuwa asiye haki huuawa na uovu. La muhimu zaidi ni kuwa Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, na wote wamkimbiliao hawatahukumiwa.

Tunaiona neema ya Mungu juu ya watu wake. Neema hii husababisha wamwaminio Bwana kuvumilia mateso katika Kristo. Kumwamini Bwana hutufanya kuwa wenye haki, na ni kwa neema yake hukomboa nafsi zetu. Tukae kwa Kristo, maana neema yake hutuwezesha. Amina.

Jumamosi njema

Heri Buberwa