Date:
11-04-2024
Reading:
Zaburi 104:24
Alhamisi asubuhi tarehe 11.04.2024
Zaburi 104:24
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.
Tutunze mazingira yetu;
Zaburi ya 104 inamsifu Mungu kwa ukuu wake kwa sababu ya uumbaji wake. Mwandishi anataja uumbaji wa Mungu na uzuri wa dunia aliyoiumba. Ni nchi yenye miti, ndege, milima, wanyama, mwezi, jua, giza, usiku, majira, bahari, misitu na vyote viijazavyo dunia.
Katika mstari tuliousoma, mwandishi anauona ukuu wa Mungu kwa matendo yake, anapokiri kuwa dunia imejaa mali zake. Yaani mwandishi anakiri kuwa Mungu ameiumba dunia, nayo dunia imejaa mali zake.
Tunakumbushwa kuwa dunia yote ni uumbaji wa Mungu. Mungu ametuumba na kutuweka tuifurahie dunia, lakini tuitunze ili iwe sehemu salama ya kuishi sisi na viumbe vyote. Tunapotunza mazingira tunatunza uumbaji wa Mungu. Amina
Uwe na Alhamisi njema.
Heri Buberwa Nteboya