“Tuwalee Watoto Katika Njia Ya Bwana," hayo ni maneno ya kutoka katika Biblia yaliyotumika katika mahubiri yaliyofanyika katika ibada ya Sikukuu ya Mikaeli na watoto iliyofanyika siku ya Jumapili tarehe 1 Oktoba 2023 katika Usharika wa KKKT Kanisa Kuu Azania Front Cathedral.
Sikukuu ya Mikaeli na watoto hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kumkumbuka malaika Mikel na watakatifu wote pamoja na watoto. Ibada hii hufanyika kwa kuongozwa na watoto wakisaidiana na walimu wao pamoja na watumishi wengine wa usharika (parish workers).
Kwa mwaka wa 2023, Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front zilifanyika ibada tatu kuadhimisha sikukuu hiyo, ibada za Kiswahili mbili na moja ya Kiingereza. Katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kuongoza shughuli zote za ibada ikiwemo kusoma litrugia, matangazo pamoja na kuongoza sala.
Akihubiri katika ibada za Kiswahili, Mwalimu Magdalena Kivulenge aliwaasa washarika, wazazi pamoja na walezi kumtafuta sana Bwana Mungu na kuhakikisha wanaishi kwenye mafundisho yake ili waweze kuwafundisha watoto wao namna ya kuishi katika ukristo na kumtumikia Mungu. “Kaa na mwanao umwonye na umwelekeze kuhusu mambo ya dunia kwa kutumia neno la Mungu.”, alisema.
“Ili watoto wetu wakae katika njia ya Bwana, jambo la kwanza sisi wazazi tuwe na neno la Mungu na tuwaelekeze watoto wetu katika kulitumia neno la Mungu. Ili tuweze kuurithi ufalme wa Mungu lazima tujishushe tuwe kama hawa watoto,” Bi Magdalena aliongeza.
Akihubiri katika Ibada ya Kiingereza, Mwalimu Kenneth Sinare aliwaasa wazazi pamoja na walezi kuwa walimu kwa watoto wao na kutumia muda mwingi katika kuwafundisha kuhusu neno la Mungu. Pia aliwaasa watoto kuwa watiifu kwa wazazi wao na jamii nzima ili waweze kukua katika maadili mema ya kikristo.
Pia katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kusema mistari ya moyo, kufanya ngonjera na kuimba nyimbo mbalimbali. Vyote hivyo vilibeba ujumbe kwa wazazi kuhusu kuwalea watoto vyema ili wakue katika maadili mema ya kikristo.
Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, Mchungaji Charles Mzinga, aliwashukuru washarika wote, walimu pamoja na wanafunzi wa shule ya Jumapili kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika sikukuu hiyo. “Niwashukuru sana wazazi na walezi kwa kuwaleta watoto, lakini niwashukuru kipekee walimu wetu pamoja na kamati ya malezi kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya kutusimamia na kuhakikisha tunavipata vile ambavyo Bwana amekusudia tuvipate katika siku hii muhimu ya watoto wetu,” alisema Chaplain Mzinga.
Mapema siku ya Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023, watoto walikusanyika katika viwanja vya Usharika ambapo walipata fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuonyesha vipaji vyao; kuchora, kuimba, kucheza pamoja na kukata keki.
---------------------------------------------------------------------------------------
MASOMO YA SIKU – MIKAELI NA WATOTO 2023
MARKO 10: 13 - 16
13 Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. 14 Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. 15 Amin, nawaambieni, yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. 16 Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.
ZABURI 25: 1 - 7
1 Ee BWANA, nakuinulia nafsi yangu,
2 Ee Mungu wangu, Nimekutumainia Wewe, nisiaibike, Adui zangu wasifurahi kwa kunishinda.
3 Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja;Wataaibika watendao uhaini bila sababu.
4 Ee BWANA, unijulishe njia zako,Unifundishe mapito yako,
5 MUniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa.
6 Ee BWANA, kumbuka rehema zako na fadhili zako, Maana zimekuwako tokea zamani.
7 Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, Wala maasi yangu.
WAEFESO 6: 1 - 4
1 Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.
2 Waheshimu baba yako na mama yako; hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,
3 Upate heri na kuishi siku nyingi katika dunia.
4 Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maagizo ya Bwana.
Baadhi ya Matukio katika Picha
Kutazama Ibada za Sikukuu ya Mikaeli na Watoto 2023:
Ibada ya Kwanza - Kiswahili >>> https://www.youtube.com/watch?v=egmfgPQFGU8
Ibada ya Pili - English >>> https://www.youtube.com/watch?v=nT55BdHnSPA
Ibada ya Tatu - Kiswahili >>> https://www.youtube.com/watch?v=iFmJqXepVWM&t=5291s
Imeandaliwa na; AZF Media Team, Oct 2023