Alhamisi asubuhi tarehe 06.07.2023
Waebrania 11:6-12
6 Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
7 Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake. Na hivyo akauhukumu makosa ulimwengu, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.
8 Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.
9 Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.
10 Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.
11 Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.
12 Na kwa ajili ya hayo wakazaliwa na mtu mmoja, naye alikuwa kama mfu, watu wengi kama nyota za mbinguni wingi wao, na kama mchanga ulio ufuoni, usioweza kuhesabika.
Kijana uwe hodari katika Imani;
Sura ya 11 inaongelea Imani, kwamba ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Kama tulivyosoma kwa sehemu, tunaona watu mbali mbali walivyofanikiwa kwa sababu ya imani. Tumemsoma Ibrahimu, Sara, na Nuhu. Wapo pia Musa, Habili, Yusufu na Yokobo. Mwandishi anarejea historia kuonesha imani yao ilivyowaweka kwa Bwana.
Katika somo tunaona haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani. Swali la kujiuliza ni kuwa tunampendeza Mungu? Kwa maana tunayo imani ya kweli? Kijana unayo Imani ya kweli katika Yesu Kristo?
Kumbuka imani bila matendo imekufa.
Siku njema.
Heri Buberwa
Mlutheri