Hii ni Pasaka
Alhamisi asubuhi tarehe 20.04.2023
Isaya 6:1-7
1 Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.
2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.
3 Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake.
4 Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi.
5 Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.
6 Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu;
7 akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.
Yesu Kristo ajifunua kwa wanafunzi wake;
Utangulizi;
Sura ya 6 ya Nabii Isaya inaelezea wito wa Mungu kwa Isaya kupeleka ujumbe wake kwa Yuda. Baadhi ya wachambuzi huona kwamba kitabu cha Isaya kingeanza na sura hii, lakini wengine huiona sura hii kama hitimisho bora la sura ya kwanza hadi ya tano. Katika sura hii Isaya ni kama anajibu swali ambalo linampa mamlaka ya kuwaambia watu wa Yuda kuhusu hukumu ya Bwana ijayo
Sura hii inaonesha mwanzo wa kazi ya Isaya kama Nabii. Hii ilikuja katika mwaka aliokufa Uzia, karibia mwaka 740 KK. Uzia alikuwa miongoni mwa wafalme wakubwa katika Yuda. Wakati wa kifo chake Waashuru walianza kuandaa silaha ambazo zingesambaratisha mataifa yote ya mashariki ya kati (Isaya 6:1, 2Fal 24:10-16)
Somo lenyewe;
Isaya anaonesha uzoefu unaoonekana, ni maono au kuonekana kwa Bwana. Aliona kwa macho yake katika hekalu huko Yerusalemu. Alimuona Bwana katika mavazi ya utukufu akikaa kwenye kiti cha enzi. Pembeni mwa Bwana walikaa maserafi, kila mmoja ana mabawa sita (6:1-2)
Maserafi wanaita kila mmoja kumsifu Mungu hadi kuitikisa misingi ya hekalu. Wanautaja utakatifu wa Mungu na kukiri utukufu wake. Wanamsifu Mungu hadi hekalu linajaa Moshi (6:3-4)
Sauti alizozisikia Isaya zilimsifu Mungu, Isaya anajiona hafai kwa jinsi alivyo kuwa katika eneo lile. Alijiona mwenye midomo michafu, mwenye dhambi, asiyefaa kumuona Bwana. Alijiona asiyestahili kumsifu Bwana kama malaika walivyofanya, alijiona kustahili kifo (6:5)
Serafi mmoja alimjia Isaya na kushika midomo yake kwa kaa la moto. Malaika huyo alisema tendo lile lilimuondolea Isaya hatia. Dhambi zake ziliondolewa, hivyo Isaya aliwekwa tayari kuongea badala ya Bwana (6:6-7).
Baada ya hapo ndipo sauti ya Bwana inaita amtume nani kazini kwake? Isaya anaitika;
Isaya 6:8
Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.Funzo;
Tunaona jinsi Isaya alivyoitwa na Bwana kazini kuanza safari ya utume. Naye aliitika kuianza kazi ya unabii, ambayo ni rejea muhimu sana leo katika Kanisa la Mungu.
Nasi leo Yesu anajifunua kwetu akituita kumwamini, kumfuata na kumtumikia. Anatuita kudumu katika safari ya Imani tukikaa kwake siku zote. Yesu anapojifunua kwetu, ni ujumbe kuwa alifufuka, yupo siku zote. Wajibu wetu ni kumpokea akae ndani yetu, nasi ndani yake ili tuwe na mwisho mwema. Amina.
Uwe na Alhamisi njema.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650