Alhamisi asubuhi tarehe 24.11.2022
Luka 20:27-40
[27]Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza,
[28]wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao.
[29]Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto;
[30]na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;]
[31]hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto.
[32]Mwisho akafa yule mke naye.
[33]Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba.
[34]Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa;
[35]lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi;
[36]wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.
[37]Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.
[38]Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake.
[39]Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema;
[40]wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo.
Uzima wa ulimwengu ujao;
Masadukayo hawakuamini katika ufufuo. Swali lao kwa Yesu lilihusu mwanamke aliyeolewa na wanaume saba, kwamba siku ya mwisho angekuwa mke wa nani? Pamoja na kwamba Swali la Masadukayo lilihusu mke aliyeolewa mara saba, lakini lilibeba dhana ya ufufuo ambayo hawakuiamini! Yesu katika kuwajibu aliwaambia kuwa mbinguni hakuna kuoa wala kuolewa. Mungu ni Mungu wa walio hai, na siyo Mungu wa wafu.
Tuiamini Injili kama mwongozo wetu kuelekea uzima wa milele. Masadukayo waliamini vitabu vitano vya Musa tu! Walikuwa na msimamo mkali, ambao kwa huo Yesu aliwaambia hawajui maandiko! Sisi tuendelee kusoma na kutafakari maandiko kama njia ya kumfuata Yesu kwa kumsikiliza.
Pia tuamini kwamba ufufuo upo, yaani Yesu atarudi kuwachukua walio hai na wafu, tayari kwa uzima wa milele.
Siku njema.