Event Date: 
20-04-2022

Usharika wa KKKT Kanisa Kuu Azania Front Cathedral umejumuika na wakristo wote ulimwenguni kusherehekea sikukuu ya Pasaka ya mwaka 2022.

Akizungumza katika ibada ya kwanza iliyofanyika Usharikani hapa, Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dk. Alex Gehaz Malasusa alisema sikukuu ya Pasaka ni muhimu sana katika maisha ya mkristo kwani ni kumbukumbu ya kushinda umauti kwa mwokozi wetu Yesu Kristo.

‘’Kufufuka kwa Yesu kunatudhihirishia sisi wakristo wa leo kwamba Yesu Kristo  ni Mungu na hakuna linalomshinda, kufufuka kwake kwa vyovyote vile kunaimarisha Imani zetu. Kama Kristo hasingefufuka basi kuhubiri kwetu kungekuwa ni bure, na Imani yetu ni bure na pia tusingekuwa na jambo la kumwelezea kwani angekufa na kutoweka katika ulimwengu huu kama wanadamu wengine.

Wapo watu wengi katika ulimwengu huu wameishi na kufanya mambo makubwa lakini walipokufa hawakurudi tena. Wapo watu wameanzisha dini na hata sasa wana wafuasi wanaowafuata lakini walikufa na hawajarudi tena. Ni mmoja tu, mtoto wa Mama Mariamu alipokufa, alifufuka, naye ni Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wetu.

Ndugu zangu hatuna Mungu wa kihistoria, tuna Mungu aliye hai na hata sasa anatusikiliza. Hatuadhimishi Pasaka tu kama sikukuu, bali tunatathimini maisha yetu na kufufuka pamoja naye,’’ alisema Baba Askofu.

Baba Askofu Malasusa pia aliongeza kusema kuwa sikukuu ya kufufuka kwa Yesu Kristo sio tu ya muujiza wa Yesu kufufuka bali ni muujiza wa maisha ya wakristo kwa kufufuka pamoja naye na kuanza maisha mapya. “Tuzizike dhambi zetu na tuanze maisha mapya ya kumpendeza Bwana wetu ambaye amefufuka hii leo,” alisema.

Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dk. Alex Gehaz Malasusa akihubiri katika ibada ya kwanza ya Pasaka katika Usharika wa KKKT Azania Front Cathedral, 17/04/2022.

Ibada ya Sikukuu ya Pasaka ilitanguliwa na kipindi cha kwaresma, pamoja na siku ya Ijumaa Kuu ambayo ndiyo siku aliyoteswa Yesu msalabani mpaka kufa kwake lakini siku ya tatu ambayo ndiyo Pasaka yenyewe Bwana Yesu alifufuka.

Katika hatua nyingine Baba Askofu Malasusa aliwataka washaarika kutokata tamaa akitolea mfano wa jiwe kubwa liliokuwa limewekwa katika kabuli la Yesu kuwa ni kuzuizi cha wao kufikia mafanikio. “Lile jiwe halipo tena, unaweza mwenyewe hapo kuzungumza moja kwa moja na Yesu bila kizuizi na bila kupitia kwa mtu yoyote. Huitaji kununua chupa ya maji au kutumbukia katika mafuta, wewe mwenyewe hapo ulipo unaweza kuzungumza na Yesu,” alisisitiza.

Katika Picha: Matukio tofauti tofauti wakati wa ibada ya Pasaka Usharikani Azania Front Cathedral 2022.

-------------------------------------------

Tazama ibada za Pasaka kupitia links zifuatazo;

  1. Ibada ya Kwanza - Kiswahili
  2. Ibada ya Pili - English
  3. Ibada ya Tatu - Kiswahili

Angalia picha za Ibada na matukio tofauti tofauti ya msimu wa Pasaka kupitia links zifuatazo:

  1. PIcha za Ibada ya Kiswahili - PASAKA
  2. Picha za Ibada ya Kiingereza - Pasaka
  3. Picha za Ijumaa Kuu

MUHIMU: Kutazama ibada na matukio mengine yanayojiri Usharikani, jiunge na AZANIA FRONT TV kupitia Ypu Tube kwa kubofya link hii. Azania Front TV