Event Date: 
07-10-2021

Wazazi waaswa kuwalea watoto katika msingi wa neno la Mungu

"Tuwapende na tuwajali watoto wetu," hayo ni maneno ya kutoka katika Biblia yaliyotumika katika mahubiri yaliyofanyika katika ibada ya Sikukuu ya Mikael na watoto iliyofanyika siku ya Jumapili tarehe 3 Oktoba 2021 katika Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront.

Sikukuu ya Mikael na watoto, hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kumkumbuka malaika Mikel na watakatifu wote pamoja na watoto. Ibada hii hufanyika kwa kuongozwa na watoto wakisaidiana na walimu wao pamoja na mtumishi wa usharika (parish worker).

Watoto wakifanya ishara wakati wakiimba katika ibada, sikukuu ya Mikael na Watoto 

Kwa mwaka wa 2021, Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront zilifanyika ibada tatu kuadhimisha sikukuu hiyo, ibada za Kiswahili mbili na moja ya Kiingereza. Katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kuongoza shughuli zote za ibada ikiwemo kusoma litrugia, matangazo pamoja na kuongoza sala.

Akihubiri katika ibada za Kiswahili, Mtumishi wa Usharika Bi FIDELIA URASSA aliwaasa washarika, wazazi pamoja na walezi kuwapenda watoto na kuwatimizia mahitaji yote muhimu ikiwa ni pamoja na kuwalea katika misingi ya neno la Mungu “Mlee mtoto wako katika njia iliyo nzuri naye hataiacha hata atakapokuwa mzee”, alisema.

“Safari ya mkristo kuelekea mbinguni inabidi kuiga maisha ya mtoto ya kuwa msikivu, mpole, myenyekevu na kutokuwa na kinyongo,”Bi Fidelia aliongeza.

Pia katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kusema mistari ya moyo, kufanya ngonjera na kuimba nyimbo mbalimbali. Vyote hivyo vilibeba ujumbe kwa wazazi kuhusu kuwalea watoto vyema ili wakue katika maadili mema ya kikristo.

Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront, Mchungaji Charles Mzinga, aliwashukuru washarika wote, walimu pamoja na wanafunzi wa shule ya Jumapili kwa kuwezesha kufanyika kwa sikukuu hiyo ambayo ni muhimu katika kuandaa kizazi bora kinachomtumikia Yesu Kristo.

Baadhi ya washarika wakifuatilia ibada ianayoongozwa na watoto 

Kuona picha zaidi:  PICHA MIKAEL NA WATOTO 2021

Kutazama ibada ya Kwanza - Kiswahili: https://www.youtube.com/watch?v=M8bsawEB7Ig

Kutazama ibada ya Pili - Kiingereza: https://www.youtube.com/watch?v=gz9dfPZuTn8

Kutazama ibada ya Tatu - Kiswahili:  https://www.youtube.com/watch?v=wxzrlW-OaDY

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ripoti hii imeandaliwa na Paulin Paul