Date: 
31-12-2024
Reading: 
2 Wakorintho 9:15

Jumanne tarehe 31.12.2024

Siku ya mwisho wa mwaka

Masomo;

Zab 102:26-28

Flp 4:19-20

*2Kor 9:15

2 Wakorintho 9:15

Mungu ashukuriwe kwa sababu ya kipawa chake, tusichoweza kukisifu kama ipasavyo.

Tumshukuru Mungu;

Paulo anawaandikia Wakorintho kukaa katika ahadi yao, kama ambavyo walikuwa wameahidi kujitoa kwa ajili ya wasiojiweza katika Yerusalemu. Anawasihi kutoa kwa hiyari, tena kwa furaha kama walivyoahidi kabla. Siyo tu kwamba watafanya kazi ya Mungu kwa kuwahudumia wahotaji, lakini itakuwa ni shukrani yao kwa Mungu. Hii inaonekana mwanzoni mwa sura ya 9;

2 Wakorintho 9:1-2

1 Kwa habari za kuwahudumia watakatifu sina haja ya kuwaandikia.
2 Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao.

-Kutoa kwao kungeweka uhusiano kati yao na wahitaji katika Kristo, kitu ambacho kingeleta utukufu wa Mungu. Hivyo sura hii ya tisa inaonesha kwamba Mungu anategemea waamini kujitoa kwa kazi yake kwa hiyari, furaha, na kwa furaha. Siyo kwa sheria, kusukumwa wala kulazimishwa.

Mtume Paulo anaelezea faida katika kumtolea Mungu. Jambo kubwa analosema Paulo ni kuitambua neema ya Mungu. Mungu hatuelekezi kumtolea kwa lazima, au kwa kujisikia, bali kwa kutambua neema yake kwetu. Kuitambua neema ya Mungu ni kutambua tulivyookolewa. Kutoa ni fursa kwa waaminio kushiriki huduma ya Mungu kwa wahitaji. Kumbe Mungu anawahudumia watu wake kupitia kwa watu wake haoaho, yaani kundi la waaminio. Hivyo kwa kutambua neema ya Mungu kwetu, tunawajibika kujitoa kwa kazi ya Mungu ili Utukufu wake uenee pote.

Mtume Paulo anakazia;

2 Wakorintho 9:6-8

6 Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.
7 Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.
8 Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;

Paulo anaposema kupanda haba na kuvuna haba ni zaidi ya utoaji. Ni dhana inayotuelekeza kutenda yatupasayo katika njia ya ufuasi ili tuwe na mwisho mwema kama kundi la waaminio. Kupanda na kuvuna haba hakuhusu fedha tu;

-Kondakta wa daladala anayerudisha chenji kwa uaminifu anapanda kwa ukarimu kuliko Mchungaji/Mwinjilisti/Mzee wa Kanisa anayeiba sadaka maana hupanda haba

-Mfagiaji wa ofisi anayewahi ofisini na kuheshimu ratiba ya kazi yake anapanda kwa ukarimu kuliko mkristo anayechukua kalamu za ofisi kupelekea watoto wake nyumbani, huyu ni mwizi, anapanda haba

-raia mwenye nguo tatu za halali hupanda kwa ukarimu kuliko mkristo tajiri fisadi n.k

Hivyo, kumtolea Mungu kwa ukarimu ni zaidi ya kutoa fedha. Ni kumuishia Bwana kwa yote tunayofanya kwa utukufu wa jina lake.

Tumshukuru Mungu;

Nimejaribu kuonesha dhana ya kumtolea Mungu kama Paulo anavyoandika kwenye sura ya 9. Kwamba Mungu anatutaka kuitambua neema yake na kumtolea kwa hiyari mali alizotupa kwa kazi yake. Tunapomtolea Mungu tunakuwa washirika katika kuitenda kazi yake. Tunapomtolea Mungu tunatoa shukrani zetu kwa Mungu ambaye hututunza na kutujalia yote. 

Mstari tuliosoma ni wito wa Paulo kwetu kumshukuru Mungu kwa sababu ya kipawa chake, tusichoweza kukisifu ipasavyo. Maana yake ni kuwa neema ya Mungu ni kubwa, haipimiki, kiasi kwamba hatuwezi kuilipia. Mwaka wa 2024 tumeumaliza kwa neema isiyo na kipimo. Tumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka huu, tukimuomba atupe mwaka mwingine wa 2025. Tutoe shukrani zetu kwa moyo tunapomshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka huu wa 2024, tukiendelea kuomba neema yake isiondoke kwetu. Amina.

Uwe na mwisho mwema wa mwaka.

Heri Buberwa Nteboya 

Mlutheri 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com