Hii ni Noeli
Jumanne tarehe 24.12.2024
Usiku Mtakatifu.
Masomo;
Zab 147:1-6. Isa 9:2-3. *Mt 1:23
Mathayo 1:23
[23]Tazama, bikira atachukua mimba,
Naye atazaa mwana;
Nao watamwita jina lake Imanueli;
Yaani, Mungu pamoja nasi.
Kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Haleluya
Injili ya Mathayo hueleza kuhusu mtoto aliyeko kwenye hori la ng'ombe. Hii ndiyo habari ya Noeli, Mungu akishuka duniani katika mwili wa Kristo. Lakini kipekee, leo tunapewa kutafakari sehemu ya Injili ya Mathayo, ambapo ananukuu unabii wa kuzaliwa kwa Yesu. Ahadi ya kuzaliwa kwa Yesu ilitolewa kupitia Nabii Isaya. Hii inadhihirika katika somo tulilosoma. Mwana aliyezaliwa analazwa horini.
Kutimizwa kwa unabii wa Isaya katika kuzaliwa kwa Yesu hakuonyeshi mwanzo wa Bwana kuwa na ahadi kwa watu wake, isipokuwa kuonyesha upeo wa Bwana kuwa na watu wake katika ahadi zake.
Leo tunasherehekea utimilifu wa ahadi ya Bwana, ya kuwa na watu wake. Tunasherehekea kuzaliwa kwa Immanuel, yaani tunasherehekea "Mungu yupo pamoja nasi"
Sikukuu ya leo, nataka tutafakari "Mungu pamoja nasi" yaani Immanuel amezaliwa.
"Mungu pamoja nasi" maana yake nini?
1.Inamaanisha wokovu.
Hili ndilo malaika alilolisema kwa Yusufu.
Mathayo 1:21
[21]Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.Ukweli ni kuwa Immanuel tu (Yesu) ndiye Mwokozi. Mpatanishi na Mkombozi wetu anakuwa mwanadamu kweli (kuwa nasi) lakini lazima awe Mungu kweli. Hivyo kuzaliwa kwa Immanueli maana yake ni wokovu toka dhambini kwa yeyote aaminiye;
Warumi 1:16
[16]Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.2.Mungu hatawaacha watu wake.
"Mungu pamoja nasi" ni neno angavu miongoni mwa watu wa Mungu. Ni neno la tumaini. Hata tuwe katika hali gani, tunajua kuwa Mungu yu pamoja nasi.
Fikiria hali labda ya kukosa ajira, kifo, talaka, kufilisika, umaskini, ugonjwa, maumivu, n.k Imanueli inamaanisha Mungu yupo pamoja nasi katika hali hizi na nyinginezo kama hizo, na zaidi. Hata katika hali hizo, upendo wa Bwana unatuzunguka. Bwana hatuachi tuumie peke yetu, yuko pamoja nasi.
Wakristo wengi duniani wanapata faraja kama Mtume Paulo anavyoandika;
Warumi 8:38-39
[38]Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, [39]wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.Immanueli amezaliwa kwa sababu Mungu yu pamoja nasi katika Yesu Kristo.
3.Hatuna sababu ya kuogopa
Kama Mungu yupo nasi, kwa ajili yetu, nani yuko juu yetu?
Warumi 8:31
[31]Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?Wakati wana wa Israeli wanapigana kurudi Kanaani, Bwana aliwatia moyo;
Kumbukumbu la Torati 31:6
[6]Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana BWANA, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.Kwa nguvu ya Mungu, tunapata nguvu na hamasa. Hivyo tusiogope.
4.Mungu ni mwenye huruma;
Yesu alipokuja duniani, alikuja katika mwili. Katika kazi yake, Kuna wakati alipata maumivu, kama mwanadamu. Yaani aliumia kama sisi, aliogopa (kumbuka kuna wakati aliomba kikombe kimuepuke).
Kwa kupata yanayotupata kama binadamu, halafu akafa kwa ajili yetu, hii ni alama ya huruma kwa mwanadamu.
Waebrania 4:15-16
[15]Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. [16]Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
Mwisho;
"Mungu pamoja nasi" ni ahadi ya Bwana kwa Kanisa. Na katika siku hii, ahadi hii ilitimia. Ahadi hii inarudiwa mara nyingi na Yesu mwenyewe;
Yohana 14:16-17
[16]Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; [17]ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.Mathayo 28:20
[20]na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.Immanueli "Mungu pamoja nasi" ilitimia alipozaliwa Bwana Yesu. Siku inakuja ambapo itatimia zaidi ya leo. Siku hiyo, tutauingia mji Mtakatifu ulioandaliwa kwa ajili yetu.
Ufunuo wa Yohana 21:3
[3]Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.Ujumbe wa "Mungu pamoja nasi" ni ujumbe wa leo, lakini pia ni tumaini la maisha yajayo. "Mungu pamoja nasi" ni salamu ya mwisho wa maandiko;
Ufunuo wa Yohana 22:21
[21]Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi nyote. Amina.
Noeli njema.
Heri Buberwa Nteboya
Mlutheri
0784 968650
Noeli 2024