Date: 
21-11-2023
Reading: 
Yoeli 2:3-11

Jumanne asubuhi tarehe 21.11.2023

Yoeli 2:3-11

3 Moto unakula mbele yao; na nyuma yao miali ya moto inateketeza; hiyo nchi inafanana na bustani ya Adeni mbele yao, na nyuma yao imekuwa jangwa tupu; naam, hakuna aliyeokoka asipatikane nao.

4 Kuonekana kwao ni kama kuonekana kwa farasi; na kama wapanda farasi ndivyo wanavyopiga mbio.

5 Kama mshindo wa magari ya vita juu ya vilele vya milima, ndivyo warukavyo; kama mshindo wa miali ya moto ilapo mabua makavu, kama mashujaa waliopangwa tayari kwa vita.

6 Mbele yao watu wanahangaika; nyuso zote zimegeuka kuwa nyeupe kwa hofu.

7 Hupiga mbio kama mashujaa; huupanda ukuta kama watu wa vita; nao huendelea mbele kila mmoja katika njia zake, wala hawapotoshi safu zao.

8 Wala hapana mmoja amsukumaye mwenzake; huendelea mbele kila mmoja katika njia yake; hujifanyizia njia kwa nguvu kati ya silaha, wala hawaachi kuifuata njia yao.

9 Huurukia mji; hupiga mbio juu ya ukuta; hupanda na kuingia ndani ya nyumba; huingia madirishani kama aingiavyo mwivi.

10 Nchi inatetemeka mbele yao; mbingu zinatetemeka; jua na mwezi hutiwa giza, na nyota huacha kuangaza;

11 naye Bwana anatoa sauti yake mbele ya jeshi lake; maana matuo yake ni makubwa sana; kwa maana yeye ni hodari atekelezaye neno lake; kwa kuwa siku ya Bwana ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye kuistahimili?

Hukumu ya mwisho inakuja;

Wakati wa Yoeli watu walikuwa katika mahitaji makubwa. Ukisoma kuanzia sura ya kwanza unaona wana wa Israeli wakivamiwa na nzige. Huu ni wakati ambao watu wa Mungu walikuwa wamerejea kutoka Yerusalemu kutoka uhamishoni. Vizazi vya nyuma hawakuwapo tena, lakini wengine walikuwa wamerudi wakijaribu kujijenga upya kimaisha. Kwa waliotegemea ardhi kwa kila kitu katika maisha yao ikiwemo kutoa sadaka, ilikuwa vizuri sana kwao.

Nabii Yoeli anaonesha kuwa watu walikuwa na shida kubwa kuliko hata hilo janga la kitaifa. Tatizo lao ni kuwa walikuwa wameridhika mno, na kuridhika kwao kulisababisha wasiwe watii kwa Mungu. Yoeli anawaasa kuamka! 

Sasa katika somo la asubuhi ya leo, Yoeli anasema kwa sababu ya kuridhika kwao, nzige hawakutokea kwa ajali, walitumwa na Mungu. Soma tena kuona katika somo;

Yoeli 2:3-4

3 Moto unakula mbele yao; na nyuma yao miali ya moto inateketeza; hiyo nchi inafanana na bustani ya Adeni mbele yao, na nyuma yao imekuwa jangwa tupu; naam, hakuna aliyeokoka asipatikane nao.

4 Kuonekana kwao ni kama kuonekana kwa farasi; na kama wapanda farasi ndivyo wanavyopiga mbio.

Hapa ndipo huwa unakuja ujumbe wa Nabii Yoeli kuwaalika watu kumrudia Bwana, ambao mara nyingi hutumika wakati wa majira ya mateso;

Yoeli 2:12-13

12 Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea;

13 rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya.

Wito wa kumrudia Bwana hudumu hata sasa, tukikumbushwa kumrudia kila wakati. Tunamrudia kwa toba ya kweli, tukilifuata neno lake. Tutende yote katika Bwana tukijua ya kuwa hukumu ya mwisho inakuja. Amina.

Jumanne njema.

 

Heri Buberwa