Date: 
11-10-2023
Reading: 
Wagalatia 3:15-22

Jumatano asubuhi tarehe 11.10.2023

Wagalatia 3:15-22

15 Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno.

16 Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.

17 Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi.

18 Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi.

19 Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe.

20 Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja.

21 Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria.

22 Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo.

Uhuru wa Mkristo;

Mtume Paulo anawakumbusha Wagalatia kuwa ahadi za Mungu kwao zilinenwa kwa Ibrahimu. Yaani Mungu alikuwa na agano nao kwa njia ya ahadi pitia kwa Ibrahim. Kwa maana nyingine anawaambia kuwa waliishi kwa sheria, ambayo walipewa na Mungu. Mstari wa 22 unahitimisha kwa kusema Yesu Kristo amefunga sheria zote kwa neno lake.

Ujumbe wa Mtume Paulo leo asubuhi ni kumfuata Yesu Kristo aliye utimilifu wa sheria. Tukiongozwa na sheria tunaangalia sheria zenyewe, bali tukimtazama Kristo tunaongozwa na neno lake, hata kuurithi uzima wa milele. Amina 

Jumatano njema

Heri Buberwa