Date: 
20-06-2023
Reading: 
Mathayo 14:22-27

Jumanne asubuhi tarehe 20.06.2023

Mathayo 14:22-27

22 Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.

23 Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.

24 Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho.

25 Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.

26 Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu.

27 Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.

Mungu hutunza Kanisa lake;

Yesu baada ya kulisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, aliwalazimisha wanafunzi wake kupanda chomboni na kutangulia ng'ambo, yeye akapanda faraghani kuomba. Walipofika katikati ya bahari chombo kikawa taabani kwa mawimbi, na usiku ule ule Yesu akawaendea kwa miguu juu ya bahari.

Ni habari ambayo ukiendelea kuisoma unaona Petro akimuomba Yesu amfuate kwa miguu juu ya maji, lakini kwa sababu ya hofu Petro akaanza kuzama. Yesu akamshika mkono akamuokoa na kuzama baharini. Yesu alipopanda chomboni upepo ukakoma.

Habari hii inatukumbusha Yesu alivyowakumbuka wanafunzi wake. Kwamba pamoja na kuwalazimisha wapande chomboni watangulie ng'ambo, bado alikuwa nao. Ndiyo maana hata bahari ilipochafuka usiku ule ule aliwaendea usiku kwa miguu juu ya bahari. Aliendelea kuwatunza.

Nasi tusiwe na shaka, kama Yesu alivyowatunza wanafunzi wake wasizame baharini, hututunza nasi siku zote. Siku njema.

 

Heri Buberwa 

Mlutheri