Date: 
19-06-2023
Reading: 
Kutoka 16:33-36

Jumatatu asubuhi tarehe 19.06.2023

Kutoka 16:33-36

33 Basi Musa akamwambia Haruni, Twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo Mana ndani yake, uiweke mbele ya Bwana, ilindwe kwa ajili ya vizazi vyenu.

34 Kama vile Bwana alivyomwagizia Musa ndivyo Haruni alivyoiweka hapo mbele ya Ushahidi, ili ilindwe.

35 Na wana wa Israeli walikula Mana muda wa miaka arobaini, hata walipofikilia nchi iliyo na watu, wakala ile Mana, hata walipofikilia mipakani mwa nchi ya Kanaani.

36 Hiyo omeri ni sehemu kumi ya efa.

Mungu hutunza Kanisa lake;

Wakati Musa anawaongoza Israeli kuelekea nchi ya ahadi, kuna wakati walimlalamikia kwa sababu ya kukosa chakula kama kile walichokula Misri;

Kutoka 16:2-3

2 Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung'unikia Musa na Haruni, huko barani;
3 wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.

Bwana alisikia kilio chao akawapa chakula jangwani. Mstari wa 35 unaonesha kuwa Mungu aliwapa chakula (Mana) ambacho walikula kwa miaka 40 wakati wa safari yao. 

Mungu alikuwa akiwakomboa Israeli toka Utumwani na kuwarejesha katika nchi ya ahadi. Walipolalamikia chakula akawapa.

Hadi hapa tunaweza kusema Mungu aliwatunza watu wake.

Mungu ametuokoa toka dhambini, hututunza kwa wema na kutupa haja zetu wakati wote. Tuendelee kumwamini na kumtegemea ili atutunze hadi uzima wa milele.

Amina.

Tunakutakia wiki njema yenye utunzaji wa Mungu 

 

Heri Buberwa