Date: 
08-03-2022
Reading: 
Mathayo 26:36-46

Hii ni Kwaresma 

Jumanne asubuhi tarehe 08.03.2022

Mathayo 26:36-46

36 Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.

37 Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.

38 Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.

39 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.

40 Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?

41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.

42 Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe.

43 Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito.

44 Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale.

45 Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi.

46 Ondokeni, twende zetuni! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia.

Tukimtegemea Bwana Tutashinda majaribu;

Baada ya Yesu kumwambia Petro kuwa atamkana mara tatu kabla ya jogoo kuwika, anamtwaa Petro na wenzake (wana wa Zebedayo) kwenda Getsemane kuomba. Wakiwa huko, wanashindwa kukesha na Yesu, aliyekuwa akiomba. Kila aliporudi alikuta wamelala.

Roho i radhi, mwili ni dhaifu;

Petro, Yakobo na Yohana walishindwa kukesha na Yesu. Usingizi uliwazidi. Katika maisha tunayoishi, tunatakiwa kumfuata Yesu kwa wakati wote. Tukae na Yesu. Tusisinzie. Tutafakari ni mambo gani yanatufanya tusinzie (tushindwe). Hayo ni majaribu tu, ambayo tukimtegemea Yesu tutayashinda yote.

Uwe na siku njema.