Date: 
28-03-2022
Reading: 
Marko 6:30-44

Hii ni Kwaresma 

Jumatatu asubuhi tarehe 28.03.2022

Marko 6:30-44

30 Na mitume wakakusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha.

31 Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula.

32 Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu.

33 Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika.

34 Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35 Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa;

36 uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula.

37 Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula?

38 Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili.

39 Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi.

40 Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini.

41 Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote.

42 Wakala wote wakashiba.

43 Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia.

44 Na walioila ile mikate wapata elfu tano wanaume.

Yesu ni mkate wa uzima;

Ishara ya kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, ni ishara inayojulikana sana. Ni ishara pekee inayopatikana katika Injili zote nne;

Mathayo 14:13-21

Marko 6:30-44 (leo asubuhi)

Luka 9:10-17

Yohana 6:1-14

Binafsi naamini siyo ishara tu, bali Somo kwa wanafunzi wa Yesu, kuliko hata makutano waliokula. Kuelewa zaidi Somo hili, vizuri kujiweka kwenye nafasi kama mwanafunzi wa Yesu; fuatilia;

Katika Injili zote, wanafunzi wanamwambia Yesu, mwishoni, jioni, baada ya huduma ya kutwa nzima, aage mkutano ili watu wakajitafutie chakula. Huu mkutano haukutarajiwa, wala kupangwa, ndio maana Yesu aliambiwa kuwa watu watawanyike.

Yesu alitumia ishara hii kama funzo (training) kwa wanafunzi wake, pale alipowajibu;

Mathayo 14:16

[16]Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula.

Ukisoma Injili ya Yohana, Yesu alikuwa akiwapa jaribio, maana alijua alilokuwa akienda kulifanya;

Yohana 6:5-6

[5]Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula?
[6]Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda.

Turudi kwenye swali;

Kwa nini Yesu aliwaambia wanafunzi wawape watu chakula?

1. Watu ni wahitaji.

Yesu alitaka kuwafundisha wanafunzi kuwa, katika utume wao, lazima watambue kuwa, watu wanaowahudumia ni wahitaji. Wanafunzi walitakiwa wajue jinsi ya kuwasaidia wapate chakula, na sio kuwaambia waondoke!

Watu tayari wako kwa Yesu, waende wapi?

Vivyo hivyo, katika utume tulioitiwa, tunawajibika kulihudumia Kanisa la Mungu (watu) na sio kuwaacha. Kuwaambia watu wakajitafutie chakula ni sawa na Leo hii kuwaacha watu bila huduma ya neno la Mungu na Kanisa kwa ujumla.

Zaidi ya hapo, hata katika maisha ya kila siku, tunaitwa kusaidiana sisi kwa sisi. Usikubali kuona mwenzio anaumia, chukua hatua kumsaidia, hata kwa mawazo, faraja, sala n.k

Bado unawaacha wenzako wakajitafutie chakula?

Yesu anakuambia Leo, wape wewe chakula.

2. Hatujitoshelezi, yaani peke yetu hatuwezi kutimiza haja za wengine.

Wakati Yesu anakaribisha makutano, wanafunzi wanakataa. Tatizo hapa lilikuwa ni "tutawapa nini?"

Wanafunzi walichotakiwa kujua, ni kuwa katika Huduma yao, walitakiwa kumtegemea Yesu ili kuutimiza utume wao. Kitendo cha kutaka watu watawanyike, ni dhahiri kuwa waliamini kuwa walikuwa hawawezi kuwahudumia wale watu. Hawakukumbuka kuwa alipo Yesu, hawashindwi lolote. Lakini Yesu alikataa watu kuondoka, na wote wakapata chakula!

Katika maisha tunayoishi, tunahitaji Yesu atuongoze, ili tuweze kuifanya kazi yake. Haiwezekani kazi ya Mungu tukaifanya kwa nguvu zetu wenyewe. Bila Yesu hatujitoshelezi!

Ndio maana tunaambiwa kuwa Yesu ni chakula cha uzima. 

3. Yesu anajibu haja za watu wake, kadri ya mapenzi yake, kwa wakati wake.

Kwanza, ilikuwa jioni, halafu Yesu alitenda kinyume kabisa na ambavyo ingeweza kufikirika katika mazingira yale; 

-labda angeshusha mana toka juu

-labda angeshusha mkate kwa kila mtu, na ghafla kila mtu angekuwa na chakula, labda ingepunguza muda ambao ulitumika kugawa chakula.

-labda angetoa hela kinunuliwe chakula n.k

Yesu aliomba na kubariki mikate mitano na samaki wawili tu!

Watu wakaanza kuketishwa!

Unafikiri kuketisha watu elfu tano ilichukua muda gani?

Unafikiri kugawa chakula ilichukua muda gani?

Yaani watu wana njaa, toka asubuhi, lakini Yesu mwenye uwezo wa kuwalisha hata ghafla anatumia muda kiasi.

Kuwa na uvumilivu katika kumsubiri Yesu atimize haja za moyo wako. Atakujibu kwa wakati wake, kadri ya mapenzi yake. 

4. Yesu anawahudumia watu wake kupitia kwa watu.

Wanafunzi waliotaka watu watawanyike, ndio hao hao Yesu aliwatumia kugawa chakula. Hapa ndipo anawafundisha wanafunzi wake, kuwa njia ya kutatua shida za dunia iliyopotea ni kupitia watu. Yesu anatimiza haja za watu, kupitia kwa watu.

Watu ndio sisi.

Yesu anakutaka uendelee kuutangaza ufalme wake, siku zote atakazokupa kuishi. Wewe ndio unayeitwa kuhudumia wengine. Acha visingizio.

5. Rasilmali tulizonazo hazitutoshi katika mahitaji yetu ya kila siku.

Mikate mitano na samaki wawili hakika visingetosha! Lakini Yesu alivibariki vikatosha.

Pale tunapotindikiwa, tuliite jina la Yesu, hakika ataonyesha njia ya kupata tunachohitaji.

Ndugu yangu;

Tunaposema Yesu ni chakula cha uzima, ni zaidi ya chakula cha mezani. Yesu ndiye chakula kilichoshuka toka juu kwa ajili ya wanadamu wote. Kuna watu walizidi kumfuata, kwa sababu walikula na kushiba ile mikate na samaki! Na Yesu aliwaambia kuwa"nyie mnanifuata kwa kuwa mmekula mikate na samaki"

Chakula cha Mungu ni kile kilichoshuka ulimwenguni kuleta uzima, Yaani Yesu mwenyewe. Mwamini Yesu aliye chakula cha uzima, ili uupate huo uzima.

Nakutakia wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio.