Date: 
21-04-2022
Reading: 
1Wakorintho 15:1-11

Hii ni Pasaka 

Alhamisi asubuhi tarehe 21.04.2022

1 Wakorintho 15:1-11

1 Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama,

2 na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure.

3 Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko;

4 na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko;

5 na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara;

6 baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala;

7 baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote;

8 na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.

9 Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu.

10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.

11 Basi, kama ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.

Tembea na Yesu mfufuka;

Mtume Paulo anawakumbusha Wakorintho kuwa Injili aliyowahubiri tangu mwanzo ni hiyo hiyo daima, kuwa Yesu ni mwokozi, aliyekuja duniani kuokoa ulimwengu. Paulo anashuhudia kufufuka kwa Yesu, akielezea alivyowatokea watu tofauti wakiwemo mitume, kundi la watu mia tano, lakini na yeye pia.

Paulo anaondoa shaka ya imani, akihakikisha kuwa Yesu kweli alifufuka, na ndiye huwezesha watu kuitenda kazi yake kwa neema. Basi nasi yatupasa kuamini, kuwa Yesu alifufuka. Tusiishie kuamini tu, bali kumfuata daima ili tutende ipasavyo kwa neema yake. Alhamisi njema.