JUMATATU TAREHE 24/05/2021
Jumatatu ya Pentekoste;
Masomo; Zab 11:1-7, Yer 31:31-34, *1Kor 12:4-11*
1Kor 12:4-11
4 Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.
5 Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.
6 Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.
7 Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.
8 Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;
9 mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;
10 na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;
11 lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.
Kuenea kwa Roho Mtakatifu;
Kanisa la Korintho lilikuwa likihangaika na mambo mengi. Walipomuuliza Mtume Paulo juu ya karama za Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha, Paulo anawajibu kwa mjadala wa kiroho pia. Paulo anawaambia kuwa ili kuelewa mambo ya kiroho, mkristo lazima kwanza amkiri Yesu, kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu. Mkristo lazima aamini kuwa Yesu ni Bwana wa vyote na Mwana wa Mungu ambaye kifo chake kilituondoa hatiani na kutushindia dhambi, na kwa Imani hutufanya wenye haki. Hivyo msingi mkubwa kuelewa karama hizi ni kumpokea na kumwamini Yesu.
Wakristo wa Korintho hawana tofauti na wale wa sasa. Ni wale watafutao kujulikana na kuonekana, na kujiona wanazo karama za Roho Mtakatifu kuliko wenzao. Waraka kwa Wakorintho tokea mwanzo unaonesha matengano yaliyokuwepo miongoni kwa kundi. Katika sura ya 12 hadi 14 anavyoandika, inakuwa vigumu kuamini kuwa karama za Roho Mtakatifu hazikuwa sababu ya utengano Kanisani. Wakorintho waligawanyika kwa kufuata viongozi, na kiongozi aliyeonekana kuwa na karama zaidi za Roho Mtakatifu alifuatwa na wengi, kama ilivyo leo. Paulo anaandika kuonesha uhusiano kati ya karama za Roho na Roho wa kweli.
Kanisa la Korintho lilibarikiwa kwa karama, na halikuwa na upungufu wa karama (1:7) lakini wahusika hawa hawakuwa na Roho wa Mungu. Paulo anawaambia kuwa wako kwa mwili zaidi, kiasi kwamba wanakuwa mbali na Mungu (3:1-3). Katika sura ya 12 hadi 15 Paulo anaongelea dhana potofu kuhusu karama za Roho na uhusiano wake. Maneno haya yalihitajika wakati wa Paulo, na leo. Leo kila dhehebu lina mfumo wake wa kutambua na kutumia karama za Roho Mtakatifu. Tunahitaji kumuelewa Paulo anasema nini kuhusu jambo hili. Sasa tulia tujifunze, siyo kuhakiki tunachojua, bali kuangalia maeneo ambayo hatuna welevu sahihi na utii;
Karama ya Roho Mtakatifu ni nini?
Ni uwezo usio wa kawaida wenye mamlaka, anaopewa mkristo na Roho Mtakatifu, unaomwezesha kufanya mambo ya kiMungu kama sehemu ya mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Kwa kifupi, karama ya Roho Mtakatifu ni nguvu isiyo ya kawaida, ya kufanya kazi ya Mungu katika Kanisa lake.
Mtazamo wa jumla kuhusu karama za Roho Mtakatifu katika Agano jipya;
Katika waraka kwa Warumi, Mtume Paulo anaeleza kuhusu karama za Roho Mtakatifu baada ya kuwasihi waaminio kuitoa miili yao kama kama dhabihu iliyo njema kwa ibada (Rum 12:1-2). Paulo anatumia mafundisho aliyoyaandika kwenye sura 11 zinazotangulia, kuwa karama ya Roho Mtakatifu ni uwezo wa kiMungu unaomwezesha mkristo kumwabudu Bwana, kama mwili wa Kristo. Zawadi zinazotajwa (kwenye Rum 12:6-8) ni "mkate na siagi" muhimu kwa huduma za Kanisa. Paulo anawaasa wakristo kutumia karama husika kadri walivyojaliwa.
Katika somo la leo, Paulo anaangalia karama zisizo za kawaida. Baadhi ya wasomi wa Agano jipya wanaamini kuwa karama hizo zilipewa nafasi kubwa na watakatifu wa Korintho (Robert L. Bob Deffinbaugh, MTh)
Lakini ukisogea mbele, Paulo anakuja na orodha nyingine ya karama za kiroho, ambazo hazifanani na zile za kwenye somo la leo;
1 Wakorintho 12:28-30
28 Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.
29 Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?
30 Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?
Sasa tushike karama zipi?
Mitume, manabii na walimu wanaonesha kazi za ofisi ya Kanisa, zile nyingine kama kunena kwa lugha, uponyaji ishara n.k zinatajwa kuwa katika kazi ya Kanisa. Katika somo la leo, Paulo anaonesha karama ambazo baadhi wanazo, wakati kwenye mstari wa 28 hadi 30 (imenukuliwa hapo juu) Paulo anaonesha kuwa pamoja na baadhi ya watu kuwa na baadhi ya karama, siyo kila mtu anaweza.
"Kila karama iliyoorodheshwa ni uwezekano kwa wote, na uhalisia kwa baadhi".
Paulo anaandika pia;
Waefeso 4:11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;
Hapa Mtume Paulo anakazia kazi za Kanisa katika huduma kwa ajili ya Kanisa lenyewe katika kuujenga mwili wa Kristo. Karama zinazoongelewa hapa sio zile "mkate na siagi" kama zile tulizoziona kwenye Warumi 12 ambazo zinaliwezesha kumuishi Kristo, hizi za hapa ni kwa makuhani kwa ajili ya utume wao.
Pia Petro katika waraka wake ameandika kuhusu karama kwa njia mbili, zile za kuongea, na za huduma.
1 Petro 4:10-11
10 kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.
11Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.
Paulo anasisitiza wote wote wenye karama hizo kuzitumia kwa uwezo wa Roho, na sio kwa njia ya mwili. Wale wanaoongea wasiongee kwa njia yao wenyewe. Neno lao litoke kwa Mungu, liwe la Mungu. Watoao huduma vivyo hivyo.
Ziko rejea nyingi, lakini naweza kusema kuwa katika Agano jipya, hakuna orodha kamili ya karama za Roho Mtakatifu. Kila orodha ina baadhi ya karama zilizotajwa kwingine. Kuna tofauti na jinsi karama zilivyo, tena kwa mwandishi yule yule (Paulo). Kila sehemu ulipowekwa ulimi, umeorodheshwa wa mwisho. Kama huu sio ushahidi kuwa ulimi siyo wenye karama muhimu (mpangilio ukihusika) angalau inatuma ujumbe kwao waonao ulimi ndio wenye karama zaidi. Mwisho, inaonekana karama za Roho Mtakatifu zilizotajwa kwenye Agano jipya siyo idadi kamili, bali sehemu tu.
Sifa za karama za Roho Mtakatifu;
1. Hizi ni karama za Roho Mtakatifu maana hutolewa na Roho Mtakatifu
2. Ni uwezo wa kiMungu kwa ajili ya huduma katika kuujenga mwili wa Kristo
3. Karama hizi lazima zilete matokeo ya Kiroho.
4. Karama hizi hutuwezesha kutimiza wajibu tuliopewa na Mungu.
Watu wa Korintho walikuwa ni watu wa majivuno, kila mmoja akijiona bora kulingana na kiongozi wake wa kiroho. Hata leo hii, wapo wanaojiona bora kwa sababu wanazo karama zinazoonekana kwa macho. Hawa wengi wao hujiona kujitosheleza na kujiona watakatifu zaidi kuliko wengine. Paulo anasisitiza karama za Roho Mtakatifu zenye kuujenga mwili wa Kristo.
Karama hazitakiwi kuleta utengano kwenye Jamii ya waaminio. Hizi zinazoleta utengano siyo karama za Roho Mtakatifu, zinatakiwa kutafutiwa jina jingine. Karama zinatakiwa ziakisi na kusaidia waamini kumwendea na kumfuata Kristo kwa uhalisia na siyo maigizo. Karama zilijenge Kanisa na siyo kulibomoa. Karama zote zijikite katika upendo ili Kanisa lidumu katika msingi wake. Msisitizo wangu ni umoja wa Kanisa katika karama yoyote iwayo, na siyo vinginevyo.
Mwisho;
1. Karama za Roho Mtakatifu siyo kigezo cha mtu kuwa Mtakatifu. Ni neema kwa aliye na karama husika. Samsoni alichaguliwa miongoni mwa waamuzi na alikuwa na nguvu. Lakini hakuwa amekua kiroho. Alikuwa mwanadamu aliyetawaliwa na mwili. Kama Wakorintho walijipima utakatifu kwa karama za Roho Mtakatifu, walikosea. Sawasawa na leo hii.
2. Karama hizi siyo sababu ya kujivuna. Hatuwezi kujivuna kwa kitu ambacho hatukukitengeneza wenyewe. Maana yake usijitape kwa kitu ambacho umepokea tu
1 Wakorintho 4:7
7 Maana ni nani anayekupambanua na mwingine? Nawe una nini usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea, wajisifia nini kana kwamba hukupokea? Kama ni kujivuna, iwe ni katika Bwana ambaye ametuchagua na kutupa mema ya nchi.
3. Karama za Roho Mtakatifu ni msingi wa umoja na siyo mgawanyiko. Inasikitisha ilivyokuwa wakati wa Paulo, vivyo hivyo leo, yaani karama hizi ni sababu ya mgawanyiko. Yesu Kristo anatupa karama katika Katika ili tutegemeane. Hebu tutafute kulinda umoja wa Roho Mtakatifu;
Waefeso 4:3 na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Tutumie karama tulizopewa kulinda umoja wetu na siyo kutengana.
4. Karama hizi lazima ziangaliwe kwa undani na kwa umakini. Mtu anaweza kuwa na karama akiihusisha na Kristo lakini kumbe ni tofauti na lengo husika katika Kanisa. Kila aaminiye anayo huduma yake na matunda tokana na huduma yake.
Yohana 15:16 Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.
--Kanisa la leo, anayeonekana kunena kwa lugha isiyojulikana ndiye anaonekana kuwa na karama Roho Mtakatifu. Haya ni mawazo finyu, ya muda.
Karama za Mungu zinatuelekeza na kutuwezesha kuitenda kazi ya Mungu katika kuujenga mwili wa Kristo. Hivyo basi, tunapokumbuka kuenea kwa Roho Mtakatifu, tuombe kuwezeshwa na nguvu ya Roho Mtakatifu katika kumtumikia Mungu, ili kazi zetu ziwe kwa ajili ya Utukufu wa Mungu, tukilijenga Kanisa lake, yaani mwili wa Kristo.
Nakutakia wiki njema.