Date: 
15-01-2026
Reading: 
Marko 1:9-11

Hii ni Epifania 

Alhamisi asubuhi tarehe 15.01.2026

Marko 1:9-11

[9]Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani.

[10]Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake;

[11]na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.

Ubatizo wetu;

Injili ya Marko huandika kwa ufupi kuhusu ubatizo wa Yesu kwa kulinganisha na Injili nyingine (Mt 3:13-17, Luka 3:21-22, Yn 1:29-34), lakini Injili ya Marko hutusaidia kuona moja kwa moja kutambua kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu aliyekuja akaishi na kufa katikati ya wanadamu wenye dhambi. Kwa nini? Injili hii haina maelezo mengi, inaonesha tu kwamba Yohana alimbatiza Yesu, na Mungu akamtambulisha kama mwanae mpendwa. 

Ubatizo wa Yohana;

Ili kuuelewa ubatizo wa Yesu, ni muhimu kuanza na Yohana Mbatizaji na sababu yake ya kubatiza. Ujumbe wa msingi kabisa wa Yohana ulihusu watu kutubu, na wale waliotubu dhambi zao walibatizwa kama alama ya toba. 

Marko 1:4-5

[4]Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.

[5]Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.

Lipo swali nimejiuliza;

Kwa nini Yesu ilikuwa abatizwe, wakati hakuwa na dhambi? Wakati Yohana alitangaza watu watubu na kubatizwa? Sawa, inawezekana maana hakuna asiye na dhambi. Vipi kuhusu Yesu ambaye hakuwa na dhambi?

Yesu hakuwa na haja ya kutubu maana hakuwa na dhambi. Lakini bado swali linahitaji kujibiwa; kwa nini Yesu alibatizwa?

Fuatana nami;

Yesu kubatizwa na Yohana kwenye mto Yordani ilikuwa ni mwanzo wa huduma yake (inaugural event). Kwa lugha ya leo naweza kusema ulikuwa "uzinduzi" wa huduma yake, maana yapo matukio yalitokea ambapo matokeo yake hutuonesha Yesu alikuwa ni nani na kwa nini alikuja. Matukio yaliyotokea ni kama ifuatavyo;

i. Mbingu zilifunguka.

Katika Agano la kale watu walipoona wako mbali na Mungu, waliweza kujieleza kwa Mungu na angewatokea akishuka toka mbinguni. Hii ilikuwa njia ya Mungu kuonekana kwa watu wake. 

Marko hasemi moja kwa moja kwamba mbingu zilifunguka, anasema mbingu zikapasuka. Hoja hapa ni kuwa mbingu ilidhihirisha kwamba Yesu ndiye Kristo, mwokozi wa ulimwengu. 

ii. Yesu alishukiwa na Roho Mtakatifu. 

Hii pia huonesha kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu. Haimaanishi kuwa alikosa sifa ya kuwa Mwokozi, bali ilitokea kwa ajili ya ukamilifu wa kuanza huduma yake kama ilivyotabiriwa;

Isaya 61:1-2

[1]Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.

[2]Kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;

Pia Roho alimshukia ili kudhihirisha ahadi hii;

Isaya 11:1-2

[1]Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.

[2]Na roho ya BWANA atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA;

iii) Baba aliongea.

Wakati matukio mawili hapo juu yakijieleza, tukio la tatu linakuja kama hitimisho, maana Mungu anamtangaza Yesu kama mtoto wake. Jambo hili hili lilitokea zaidi ya mara moja;

Marko 9:7

[7]Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.

Sasa basi,

Nilikuwa naeleza ni kwa nini ilikuwa Yesu abatizwe, ambapo tumeona mbingu zikifunguka, kushuka kwa Roho Mtakatifu na Baba akimtambulisha mwana. Ilikuwa ni mwanzo wa huduma yake.

 

-Yesu alikwenda kubatizwa ubatizo wa wenye dhambi, kwa sababu alikuja kwama mwanadamu, akaishi na kufa katikati ya wenye dhambi ili kuwaokoa. Kubatizwa kwa Yesu kulionesha unyenyekevu wake (Mt 3:15) na utayari wake wa kuwakomboa wanadamu.

Ubatizo wetu;

Kama tulivyoona, ubatizo ulikuwa ni hatua ya Yesu kuanza kazi yake. Ubatizo ulikuwepo, ndiyo maana haiandikwi aliyembatiza Yohana ni nani, bali wameandika kuonesha ubatizo wa Yesu. Kwa maana hiyo, Wakristo hubatizwa na kwa njia hiyo humpokea Yesu Kristo. Hadi hapa ni muhimu kukumbushana kuishi ahadi ya ubatizo wetu, maana ubatizo ni alama ya kumpokea Yesu.

-Ubatizo ni wokovu kamili;

Tunapobatizwa tunaokolewa. Uhakika huu unatokana na ahadi ya ubatizo tunayokiri wakati wa kubatizwa. Huwa tunamkataa shetani, na mambo yake yote, na kazi zake zote. Tunajitoa kuwa wake, na kumtumikia kwa uaminifu hadi kufa. Halafu mtu anatoka hapo anaambiwa hujaokoka anakubali! Elewa maana ya ahadi ya ubatizo uliyokiri siku ya Kipaimara. Uliokoka. Kama ulienda kinyume na hapo tengeneza na Bwana, anakungoja na kukuita sasa.

-Ubatizo ni wa maji mengi au machache?

Ubatizo ni wa maji yenye neno la Mungu.

Yesu alibatizwa mto Yordani. Wapo wanaobatizwa baharini, mabwawa, na wengine hawana maji kwenye maeneo ya jangwa! 

Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani, yupo askari aliyeamini akabatizwa yeye na familia yake usiku ule. Usiku alibatizwa wapi? (Mdo 16)

Ipo changamoto ya waamini kuhusu ubatizo wa watoto;

Hivi mtoto akiumwa unasubiri akue aelewe ndipo umpeleke hospitali? Kwa nini unampeleka bila ridhaa yake?

Mbona tunawapeleka watoto shuleni (na sisi tulipelekwa) wakiwa wadogo, hatusubiri wakue waamue kusoma?

Kama hayo yote tunawafanya, kwa nini tusiwalete kwa Yesu ambapo ni salama kuliko mahali popote? 

Jambo la msingi tuwalee watoto katika njia ya kuiishi ahadi ya ubatizo, maana huwa tunakiri kwa niaba yao wanapobatizwa. 

Mwisho;

-Ubatizo umetuleta kwa Yesu, na kwa kubatizwa tumetangaziwa ondoleo la dhambi.

-Ahadi ya ubatizo ni wokovu kamili. Simama katika ahadi ya ubatizo uliyokiri ulipobatizwa, uache kutangatanga kama kondoo asiye na Mchungaji.

-Tusiwe kama Wayahudi walioohoji mamlaka ya Yesu, wakapata kigugumizi juu ya ubatizo wa Yohana, yaani ule ubatizo wa toba, (Luka 20:1-8) mbele ya Yesu, bali tuamini katika ubatizo wetu, tuishi ahadi yetu ya ubatizo kila mmoja, tukiamini kuwa kwa kubatizwa tumekuwa wana wa Mungu. Amina

Siku njema

Heri Buberwa Nteboya 

 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com