Date: 
18-07-2025
Reading: 
2 Mambo ya nyakati 30:13-20

Ijumaa asubuhi tarehe 18.07.2025

2 Mambo ya Nyakati 30:13-20

13 Basi wakakusanyika Yerusalemu watu wengi ili kuifanya sikukuu ya mikate isiyochachwa katika mwezi wa pili, kusanyiko kuu sana.

14 Wakainuka, wakaziondoa madhabahu zilizokuwamo Yerusalemu, nazo madhabahu za kufukizia wakaziondoa, wakazitupa katika kijito Kidroni.

15 Kisha wakaichinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, nao makuhani na Walawi wakatahayarika, wakajitakasa, wakaleta sadaka za kuteketezwa nyumbani mwa Bwana.

16 Wakasimama mahali pao kwa taratibu yao, sawasawa na torati ya Musa, mtu wa Mungu; nao makuhani wakainyunyiza damu, waliyoipokea mikononi mwa Walawi.

17 Kwa maana kulikuwa na wengi katika kusanyiko ambao hawajajitakasa; kwa hiyo Walawi wakamchinjia pasaka, kila mtu asiyekuwa safi, ili kuwatakasa kwa Bwana.

18 Kwani wingi wa watu, naam, wengi wa Efraimu, na wa Manase, na wa Isakari, na wa Zabuloni, hawakujisafisha, lakini wakala pasaka, ila si kama ilivyoandikwa. Naye Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, Bwana mwema na amsamehe kila mtu,

19 aukazaye moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa babaze, hata ikiwa si kwa utakaso wa patakatifu.

20 Bwana akamsikia Hezekia, akawaponya watu.

Tuhurumiane katika Kristo;

Sura ya 30 ambayo tumesoma sehemu yake inasimulia habari ya Mfalme Hezekia kurejesha na kusherehekea Pasaka katika Yerusalemu akiwakaribisha Israeli na Yuda wote kushiriki kwa pamoja. Maudhui ya sura hii ni toba, umoja, na rehema ya Mungu, kwa maana watu wanaalikwa kumrudia Bwana na kupata msamaha. Hezekia alitambua umuhimu wa toba akawatuma watendakazi katika Israeli na Yuda, bila kusahau Manase na Efraimu kuwaalika watu wote kwa ajili ya Pasaka katika Yerusalemu.

Pasaka ilikuwa imeachwa kwa sababu hakukuwa na makuhani wa kutosha na watu walikuwa hawakushanyiki tena Yerusalemu.

Somo tulilosoma ndipo linaonesha watu wakikushanyika katika Yerusalemu, wakaondoa ibada za sanamu, wakamwabudu Mungu kwa kuisherehekea Pasaka kama agizo la Bwana lilivyokuwa. Watu waliitikia wito wa Hezekia wakamrudia Bwana, wakitoa sadaka na kusherehekea Pasaka. Yesu Kristo ndiye mwanakondoo wa Pasaka aliyejitoa sadaka kwa ajili yetu, hutuita kumuamini na kutuhurumia daima. Amina

Ijumaa njema

Heri Buberwa