Hii ni Pasaka
Ijumaa asubuhi tarehe 09.05.2025
Yohana 10:11-16
11 Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.
12 Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.
13 Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.
14 Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi;
15 kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.
16 Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
Yesu ni Mchungaji mwema;
Zamani za Agano la kale, kazi ya kuchunga makundi ya wanyama ilifanywa na wachungaji waliokaa kondeni kwa kupeana zamu. Wachungaji hawa walikuwa na wajibu wa kulisha, kupeleka wanyama visimani kunywa maji, kuangalia na kuhudumia wanyama wagonjwa. Kama mifugo ingevamiwa na simba, au wanyama wengine hatari, wachungaji walihatarisha maisha yao kwa kuokoa wanyama hao.
Katika somo la asubuhi ya leo, Yesu anasema yeye ni Mchungaji mwema kwa kuwa anawajali wanaomwamini, kiasi cha kuutoa uhai wake kwa ajili yao. Kristo pekee ndiye aliyeutoa uhai wake kwa ajili ya wengi na siyo mwingine yeyote! Hakika huyu ndiye Mchungaji mwema! Mwamini sasa uokolewe. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa