Date: 
01-05-2025
Reading: 
Isaya 33:13-15

Hii ni Pasaka

Alhamisi asubuhi tarehe 01.05.2025

Isaya 33:13-15

13 Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu.

14 Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?

15 Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu.

Yesu ajifunua kwetu;

Somo la asubuhi hii ni ahadi ya Mungu kwa Taifa lake, ahadi ambayo ni unabii wa kukombolewa kutoka kwa watesi. Israeli wanapewa unabii wa kukombolewa kutoka uhamishoni. Somo linaanza kwa kuwatambua kama "walio mbali" yaani uhamishoni, wenye dhambi, wasiomcha Mungu. Somo linamtaja Mungu kama mwenye haki, asiyependa dhuluma, asiyepokea rushwa, achukiaye uovu.

Somo linahusu ahadi ya Israeli kukombolewa kutoka Babeli. Mungu alijifunua kwao kwa njia ya unabii, baadaye akawatoa huko uhamishoni. Leo Mungu anajifunua kwetu kwa njia ya Yesu Kristo, tukikumbushwa kumwamini na kumpokea katika maisha yetu. Yesu Kristo mfufuka anatuita kukaa kwake daima, ili atupe mwisho mwema. Amina

Alhamisi njema

 

Heri Buberwa