Date: 
03-04-2025
Reading: 
Isaya 28:23-29

Hii ni Kwaresma 

Alhamisi asubuhi tarehe 03.04.2025

Isaya 28:23-29

23 Tegeni masikio, sikieni sauti yangu, sikilizeni mkasikie neno langu.

24 Je! Mwenye kulima alima daima, ili apande? Afunua daima madongoa ya nchi yake, na kuyavunja?

25 Akiisha kuulainisha uso wa nchi yake, je! Hamwagi huko na huko kunde, na kutupa-tupa jira, na kuitia ngano safu safu, na shayiri mahali pake palipochaguliwa, na kusemethi karibu na mipaka yake?

26 Kwa maana Mungu wake anamwagiza vizuri na kumfundisha.

27 Kwa maana kunde zile hazipurwi kwa chombo kikali, wala gurudumu la gari halipitishwi huko na huko juu ya jira ile, bali kunde zile hupurwa kwa fimbo, na jira ile kwa ufito.

28 Ngano ya mkate husagwa; kwa maana haipuri siku zote bila kukoma; na ingawa gurudumu la gari lake na farasi wake huitawanya ngano ile, haisagi.

29 Hayo nayo yatoka kwa Bwana wa majeshi, mwenye shauri la ajabu, apitaye wote kwa hekima yake.

Tutunze uumbaji (mazingira)

Mungu aliwapa mausia mengi wana wa Israeli kupitia kwa Nabii Isaya kabla ya kwenda uhamishoni. Somo la asubuhi ya leo ni sehemu ya mausia hayo, ambapo Israeli wanaelekezwa kufanya kazi kwa kutumia ardhi waliyopewa. Wanaelekezwa jinsi ya kutumia ardhi ili iwape mavuno bora. Utaona ni maelekezo ya jinsi ya kupata ngano safi, zao likilokuwa likilimwa nao wakati ule.

Msisitizo kwa Israeli katika somo ni kufanya kazi kwa bidii, kwa kutumia rasilmali ya ardhi waliyopewa. Kwa njia hii walikuwa wanaelekezwa wasiwe wavivu, maana uvivu ni dhambi. Nasi tunaitwa kuwa na bidii katika kazi, na katika kazi zetu tuhakikishe tunatunza uumbaji wa Mungu. Amina

Alhamisi njema 

Heri Buberwa