Date: 
01-02-2025
Reading: 
Luka 6:30-35

Hii ni Epifania 

Jumamosi asubuhi tarehe 01.02.2025

Luka 6:30-35

30 Mpe kila akuombaye, na akunyang'anyaye vitu vyako, usitake akurudishie.

31 Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo.

32 Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao.

33 Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo.

34 Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile.

35 Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu.

Mungu hana upendeleo;

Leo tunasoma juu ya Upendo kwa adui. Ukisoma kuanzia mstari wa 27 Yesu anafundisha juu ya kuwapenda adui na kuwaombea wanaotuudhi. Yesu anaendelea kufundisha juu ya kutolipiza kisasi. Ndipo linakuja somo tulilolisoma, ambalo linaelekeza kutenda mema kwa wengine kama Yesu mwenyewe. Mstari wa 35 unasisitiza upendo kwa adui na kutenda mema pasipo kutegema malipo. 

Yesu anatukumbusha kuwapenda adui zetu, bila upendeleo. Yeye alifundisha wote, akawahubiri na kuponya wote bila upendeleo. Hivyo tunapoelekezwa na kukumbushwa kupendana, tunafanya alilolifanya Yesu, yaani kuwapenda watu wote. Tupendane, tusipendeleane. Amina

Jumamosi njema

Heri Buberwa