Jumanne asubuhi tarehe 26.11.2024
Yeremia 31:15-20
15 Bwana asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako,
16 Bwana asema hivi, Zuia sauti yako, usilie, na macho yako yasitoke machozi; Maana kazi yako itapata thawabu, nao watakuja tena toka nchi ya adui; Ndivyo asemavyo Bwana.
17 Tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema Bwana; na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe.
18 Hakika nimemsikia Efraimu, akijililia hivi, Umeniadhibu, nami nikaadhibika, kama ndama asiyeizoelea nira; unigeuze, nami nitageuzwa; kwa maana wewe u Bwana, Mungu wangu.
19 Hakika baada ya kugeuzwa kwangu, nalitubu; na baada ya kufundishwa kwangu, nalijipiga pajani; nalitahayarika, naam, nalifadhaika, kwa sababu naliichukua aibu ya ujana wangu.
20 Je! Efraimu siye mwanangu mpendwa? Je! Siye mtoto apendezaye? Maana kila nisemapo neno juu yake, ningali nikimkumbuka sana; kwa sababu hiyo moyo wangu unataabika kwa ajili yake; bila shaka nitamrehemu, asema Bwana.
Baada ya maisha haya, uzima wa milele;
Yesu alipozaliwa, mtawala Herode alikuwa na wasiwasi juu ya Yesu aliyezaliwa. Akawatuma Mamajusi wakamletee habari kuhusu mtoto Yesu. Lakini Mamajusi walitokewa na malaika wa Bwana akawaelekeza kutorudi kwa Herode maana alitaka kumuangamiza mtoto. Herode alikasirika sana. Hii ni sehemu ya historia aliyopitia Yesu Kristo katika kutukomboa sisi. Herode aliagiza watoto wote chini ya miaka 2 kuuawa, na sehemu ya maneno katika somo tulilolisoma yamenukuliwa na Mathayo kama alivyotabiri Isaya.
Soma hapa;
Mathayo 2:16-18
16 Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.
17 Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema,
18 Sauti ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.
Tukitafakari zaidi, tunachosoma asubuhi ya leo ni sauti ya Mungu kupitia kwa nabii Yeremia ikisema juu ya mtu anayelia kwa ajili ya toba na faraja mbele za Bwana. Anaiona hasira na adhabu ya Bwana, lakini anaomba rehema ya Bwana.
Yeremia alikuwa anatabiri rehema juu ya Israeli waliokuwa mateka Babeli. Pamoja na kurudi kwa shangwe, walitakiwa kumcha Bwana aliyewapa neema, yaani aliyewaokoa.
Maisha yetu yana hatua nyingi ambazo kama siyo Bwana hatuwezi kufanya lolote. Tunaweza yote kwa neema yake. Hivyo tudumu katika neema hii tukizidi kuomba rehema ya Bwana juu yetu siku zote, ili baada ya maisha haya tuwe warithi wa uzima wa milele. Amina
Uwe na siku njema.
Heri Buberwa