Date: 
12-11-2024
Reading: 
Ufunuo wa Yohana 19:1-8

Jumanne asubuhi tarehe 12.11.2024

Ufunuo wa Yohana 19:1-8

1 Baada ya hayo nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, sauti kubwa mbinguni, ikisema, Haleluya; wokovu na utukufu na nguvu zina BWANA MUNGU wetu.

2 kwa kuwa hukumu zake ni za kweli na za haki; maana amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uasherati wake, na kuipatiliza damu ya watumwa wake mkononi mwake.

3 Wakasema mara ya pili, Haleluya. Na moshi wake hupaa juu hata milele na milele.

4 Na wale wazee ishirini na wanne, na wale wenye uhai wanne, wakasujudu na kumwabudu Mungu, aketiye katika kile kiti cha enzi, wakisema, Amina, Haleluya.

5 Sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Msifuni Mungu wetu, enyi watumwa wake wote, ninyi mnaomcha, wadogo kwa wakuu.

6 Nikasikia sauti kama sauti ya makutano mengi, na kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi yenye nguvu, ikisema, Haleluya; kwa kuwa Bwana Mungu wetu, Mwenyezi, amemiliki.

7 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.

8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing'arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.

Mwenye kuvumilia hata mwisho ndiye atakayeokoka;

Yohana anafunuliwa sauti kama ya makutano wengi wakimsifu Mungu, wanamsifu na kusema Haleluya, wokovu na nguvu zina Bwana Mungu wetu. Yohana anafunuliwa kuwa hukumu za Mungu ni za haki daima. Anafunuliwa wazee ishirini na wanne na wale wenye uhai wanne wakisujudu na kumwabudu Mungu aketiye kwenye kiti chake cha enzi. Sauti inatoka kwenye kiti cha enzi ikiwaita watu wote kumsifu Mungu.

Anachofunuliwa Yohana ni shangwe mbinguni. Anapewa utukufu Mungu anayemiliki. Kwa mujibu wa ufunuo wa Yohana, ipo mbingu kwa ajili ya wote waaminio baada ya kumaliza kazi hapa duniani. Mbingu hiyo tutaingia kwa kumwamini na kumfuata Yesu, na huko ndipo tutamsifu pasipo kukoma. Tuvumilie katika imani ili tuufikie huo mwisho mwema, maana atakayevumilia hata mwisho ndiye atakayeokoka. Amina.

Jumanne njema

 

Heri Buberwa 

Mlutheri