Event Date: 
06-10-2024

Siku ya Jumapili, tarehe 06/10/2024, Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front uliadhimisha kilele cha sikukuu ya mavuno ya mwaka 2024, maadhimisho ambayo hufanyika kila mwaka ili kutoa fursa kwa washarika kumtolea Mungu sehemu ya matunda au mavuno ya kazi walizozifanya kwa kipindi cha mwaka mzima.

Ibada ya kusherehekea sikukuu hii ya mavuno kwa mwaka huu imefanyika katika viwanja vya usharika wa Kanisa Kuu Azania Front ikihudhuiriwa na mamia ya washarika waliojitokeza wakiwa na mavuno yao tayari kwa kumtolea Mungu. Somo: Mwanzo 4:7; Nguvu Ya Imani Katika Yesu Kristo (Mavuno)

Ibada hiyo imeongozwa na Msaidizi wa Baba Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Chediel Lwiza, akiambatana na Mchungaji Kiongozi wa Usharika Chaplain Charles Mzinga na Mchungaji Joseph Mlaki; wakisaidiwa na Watumishi wote wa Usharika pamoja na Wazee wa Kanisa. 

Akizungumza wakati wa Ibada hiyo, Dean Chediel Lwiza aliwakumbusha washarika wa Azania Front Cathedral kuwa uhusiano wa Mungu na sadaka ni wa moja kwa moja na kwamba hauna mkato na kwamba sadaka ina nguvu ya kutambulisha moyo wa mtu na kumsogeza karibu zaidi na Mungu. “Mungu akishaona ile sadaka, kitu cha pili anachokiona ni moyo wako, na siyo kitu kingine, alisema Dean Chediel Lwiza. “Hata kama umeleta ua kutoka kwenye bustani yako, Mungu ana uhusiano na hilo ua moja kwa moja; lakini anapotoka kwenye ua anakuja kwa yule aliyebeba ili aone moyo wake…. Hii maana yake ni kwamba sadaka inatambulisha moyo wako”.

Dean Lwiza pia alisisitiza kuwa sadaka ina nguvu ya kumkutanisha mtu na Mungu moja kwa moja, akitolea mfano wa Kaini na namna ambavyo Mungu alifuatilia sadaka yake.  “Umeleta sadaka hapa, mimi sitafuatilia, Chaplain hatafuatilia, wazee wa kanisa hawatafuatilia, ila Mungu mwenyewe atafuatilia,” alisema Dean Lwiza.

Dean Lwiza aliongeza kusema kuwa sadaka yoyote ile inatolewa kwa kuwa na moyo wa upendo, kwa kuwa na imani pamoja na moyo wa utiifu. Dean Lwiza pia aligusia madhara ya sadaka kuwa inaweza kuondoa uhai wa mtu na pia kuondoa fursa au nafasi ya mtu.

Ibada ya sikukuu ya mavuno ilitanguliwa na maandamano mafupi na utoaji wa sadaka pamoja na mavuno huku ikihitimishwa kwa mahubiri kutoka kwa Dean Chediel Lwiza na mwisho kabisa ukifanyika mnada wa bidhaa au mavuno yaliyokuwa yamewasilishwa na washarika.

Pia Kwaya kutoka Usharika wa KKKT Chang’ombe iliungana na Kwaya za Usharika wa Azania Front Cathedral katika kuipamba ibada hiyo kupitia tungo mbalimbali za kumtukuza Bwana Mungu wetu.

Angalia picha zaidi hapa chini:

Matukio mbalimbali katika picha wakati wa ibada ya Sikukuu ya Mavuno iliyofanyika katika viwanja vya Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, tarehe 06/10/2024. Picha: AZF Media Team.

Tazama ibada: https://www.youtube.com/watch?v=yQK_fzNeAp0

-------------- MWISHO -----------------