Date: 
03-08-2024
Reading: 
Yeremia 6:22-26

Jumamosi asubuhi tarehe 03.08.2024

Yeremia 6:22-26

22 Bwana asema hivi, Tazama, watu wanakuja, wakitoka katika nchi ya kaskazini; na taifa kubwa litaamshwa, litokalo katika pande za mwisho wa dunia.

23 Washika upinde na mkuki; ni wakatili, hawana huruma; sauti yao huvuma kama bahari, nao wamepanda farasi zao; kila mmoja kama mtu wa vita amejipanga juu yako, Ee binti Sayuni.

24 Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake.

25 Msitoke kwenda mashambani, wala msitembee njiani, kwa maana upanga wa adui uko huko; hofu ziko pande zote.

26 Ee binti wa watu wangu, ujivike nguo ya magunia, na kugaagaa katika majivu; fanya maombolezo, kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, maombolezo ya uchungu mwingi; maana mwenye kuteka nyara atakuja juu yetu ghafula.

Mungu hupendezwa na mwenye moyo wa toba;

Yeremia anatoa taarifa ya kuvamiwa kwa Yerusalemu. Kengele inapigwa kona zote kutoa habari hii. Mungu anawaita watu wa Yuda kurudi katika njia ya haki lakini wanakataa, hivyo sadaka zao hazipokelewi. Somo linaonesha jeshi kutoka Kaskazini kuvamia nchi, lakini bado watu hawasikii. Ni watu waliokataa kuisikia sauti ya Mungu, hivyo wanapewa habari ya kuvamiwa. 

Tunaona kwamba tunaweza kupatwa na mambo mabaya tunapokataa kuitii sauti ya Mungu kupitia neno lake. Somo la leo linatukumbusha kuisikia sauti ya Mungu na kumgeukia. Tumesoma watu wa Yuda wakiitwa kutubu ili wasiwekwe mateka. Ni wito kwetu kumcha Bwana kwa kufanya toba ili tusianguke dhambini. Amina

Jumamosi njema.

 

Heri Buberwa