Date: 
01-08-2024
Reading: 
Matendo ya mitume 3;17-23

Alhamisi asubuhi tarehe 01.08.2024

Matendo ya Mitume 3:17-23

17 Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda.

18 Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo.

19 Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana;

20 apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;

21 ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.

22 Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi.

23 Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake.

Mungu hupendezwa na mwenye moyo wa toba;

Petro na Yohana walikuwa wakiingia hekaluni kusali, wakamkuta kiwete amekaa mlangoni mwa hekalu. Yule kiwete alinyoosha mikono kupata kitu kwao, lakini Petro akimkazia macho, akasema tunakupa tulicho nacho, yaani kumuombea uponyaji kwa jina la Yesu Kristo. Yule kiwete akapona. Sasa yule kiwete akawashika Petro na Yohana, hakuwaacha. Akaingia nao hekaluni, na watu wengi wakabaki na mshangao.

Petro alipoingia hekaluni akaona umati mkubwa ukiendelea kushangaa kwa lililotokea, ndipo akaanza kuhutubia akiwaambia kiwete ameponywa na Yesu waliyemkataa, wakamtesa na kumtundika msalabani kumuua! Ndipo kwenye somo anawaambia walifanya hivyo (yaani kumkataa na kumuua Yesu) bila kujua, hivyo kuwasihi watubu ili Kristo awasamehe. Anawaambia kuwa wasipotubu wataangamizwa.

Tunaalikwa kuishi maisha ya toba ili tuwe na mwisho mwema. Amina

Alhamisi njema

Heri Buberwa