Date: 
20-05-2024
Reading: 
Matendo 8:14-17

Hii ni Pentekoste;

Jumatatu ya Pentekoste;

Tarehe 20.05.2024;

 

Masomo;

Zab 119:49-50

1Kor 12:4-11

*Mdo 8:14-17

Matendo ya Mitume 8:14-17

14 Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana;

15 ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu;

16 kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu.

17 Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu kwa kila aaminiye;

Kitabu cha Matendo ya Mitume huwa kinao ujumbe wa Roho Mtakatifu kama ahadi kwa wote waaminio kama tulivyosoma katika somo hilo hapo juu. Haina ubishi kwamba Roho Mtakatifu huhitaji waaminio ili kazi ya huyo Roho kudhihirika. Watu wa Samaria na makundi mengine yote walikuwa na uwezekano wa kubatizwa na kumpokea Roho Mtakatifu kwa pamoja. Sasa ni kwa nini hawakumpokea Roho Mtakatifu walipobatizwa? Wapo wachambuzi wanaosema Mungu huenda alitaka kujenga uhusiano kati ya watu wa Yerusalemu Petro na Yohana, na wale wa Samaria. Hii inabaki mshangao kwa wasomaji na wachambuzi wote.

Sisi lazima tuendelee mbele, kwamba kuchelewa kwa Roho Mtakatifu kama tulivyosoma kwa watu wa Samaria, kwaweza kuwa funzo kwetu kwa Roho Mtakatifu kuwa Mpatanishi miongoni mwa watu wa mataifa yote, na watu wa makundi yote. Luka (mwandishi) haonekani kuweka wazi ajenda ya Roho Mtakatifu kwenye hii sura ya nane, lakini haituzuii sisi kufahamu kuwa kila mmoja anaweza kuipokea nguvu ya Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu, yaani Mungu mwenyewe.

Kwa maana nyingine somo la leo, yaani Mdo 8:14-17 ni mwaliko wa uanafunzi kwa wote. Kwa kuzingatia historia ya Wayahudi na Samaria, kuchelewa kwa Roho Mtakatifu ni funzo kwa waamini kutambua kazi ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anaonekana kuwa wa muhimu, ndiyo maana inaandikwa walibatizwa lakini bila kumpokea huyu Roho. Hivyo walikosa kitu muhimu. Walimkosa Roho Mtakatifu, Mungu mwenyewe. Kwa hiyo kwa kumwamini Yesu Kristo, na kwa njia ya ubatizo, tulimpokea Roho Mtakatifu ambaye hututunza na kutuongoza daima. 

Kuwepo kwa Petro na Yohana katika Samaria kunaweza kutafsiriwa kama upatanisho na kuleta amani miongoni mwa mataifa. Kazi ya mision leo kuna mahali inahitaji upatanisho kwa watu wa Mungu. Katika somo, Petro na Yohana hawakuwa na mtazamo hasi juu ya Samaria, bali waliwawekea mikono na kujenga ushirika kati ya watu wa Yerusalemu na Kanisa la Samaria. Hivyo inaonekana Roho Mtakatifu alihitajika kupatanisha watu wa Yerusalemu na Samaria. Palipokuwa na Roho Mtakatifu waamini pia walibadilika, na kwa hilo naweza kusema kuwa "imani katika Kristo siyo timilifu bila Roho Mtakatifu kati ya watu wake". Somo tulilosoma linaonesha watu wakimpokea Roho Mtakatifu. Sehemu nyingine imeandikwa kuonesha jambo hilihili, kuwa Roho Mtakatifu alibadilisha watu, hebu soma habari hii katika kitabu hicho hicho cha Matendo ya Mitume;

Matendo ya Mitume 19:1-6

1 Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;
2 akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.
3 Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.
4 Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.
5 Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
6 Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.

Tumesoma Petro na Yohana wakiwawekea mikono watu wa Samaria. Pia hapo juu Paulo anawawekea mikono watu na wanampokea Roho Mtakatifu. Watu kuwekewa mikono na Paulo, Petro na Yohana inaonesha kuwa Roho Mtakatifu alishuka kwa ajili ya wote. Ni kwa sababu wote waliowekewa mikono walimpokea Roho Mtakatifu bila kujali tofauti zao. Sifa ilikuwa ni kumwamini Yesu Kristo. 

Roho Mtakatifu kwa kila aaminiye;

Somo linaonesha Petro na Yohana kuwawekea mikono watu wa Samaria. Imeandikwa hivyo kulingana na mazingira ya wakati ule. Mitume ndiyo walikuwa kazini kuhubiri Injili. Hatuhitaji kwenda Yerusalemu kumpokea Roho Mtakatifu, mawazo ya namna hiyo ni uzushi, uongo. Luka anaelezea misioni ya Mungu kupitia kwa Mitume, misioni ambayo leo inatimia kupitia kwa wachungaji wetu. Kwamba tunapomwamini Yesu, wakatubatiza na kutuwekea mikono tunampokea Roho Mtakatifu. Kila anayebatizwa anampokea Roho Mtakatifu maishani, ambaye hutusaidia katika mambo yote tufanyayo. 

Roho Mtakatifu huyu ni Mungu kamili, kwa wote. Ndiyo maana Petro, Yohana, Paulo na wengineo walipowekea watu mikono walimpokea huyu Roho. Kumbe Roho Mtakatifu hachagui! Ni wetu sote, tunaye. Kuna ambao wanatembea na roho mtakatifu mfukoni, wakianza maombi wanamuachilia! Sijajua ni mwanadamu gani anaweza kuachilia Roho Mtakatifu! Maana hata wachungaji wetu wanatuombea nguvu ya Roho Mtakatifu toka kwa Mungu mwenyewe, na tunapokea kwa imani. Roho Mtakatifu ni wa wote, tunaye.

Tusimzimishe Roho;

Yapo mafundisho kwamba ukitenda dhambi Roho Mtakatifu anaondoka. Roho Mtakatifu hawezi kuondoka maana ni ahadi kwetu daima. Tunapomkosea Mungu tunamzimisha Roho, ndiyo maana Mtume Paulo anatuasa;

1 Wathesalonike 5:19 Msimzimishe Roho;

Roho Mtakatifu hutuongoza kutenda kwa Utukufu wa Mungu, hivyo basi tusimzimishe huyo Roho akaaye kwetu daima.

Mwisho;

Kama tulivyoona, watu waliwekewa mikono wakampokea Roho Mtakatifu. Hivyo Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya wote. Tunaalikwa kudumu katika imani tukiongozwa na Roho Mtakatifu aliye Mungu kamili, maana yuko ndani yetu daima. Amina.

Tunakutakia wiki njema.

 

Heri Buberwa Nteboya 

Jumatatu ya Pentekoste 2024