Date:
02-03-2024
Reading:
Waebrania 13:22-25
Hii ni Kwaresma
Jumamosi asubuhi tarehe 02.03.2024
Waebrania 13:22-25
22 Lakini nawasihi, ndugu, mchukuliane na neno hili lenye maonyo maana nimewaandikia kwa maneno machache.
23 Jueni ya kuwa ndugu yetu Timotheo amekwisha kufunguliwa; ambaye, akija upesi, nitaonana nanyi pamoja naye.
24 Wasalimuni wote wenye kuwaongoza, na watakatifu wote; hao walio wa Italia wanawasalimu.
25 Neema na iwe nanyi nyote.
Mchukuliane katika upendo;
Ni sura ya mwisho ya waraka kwa Waebrania, ambapo mwandishi anaanza sura hii ya 13 kwa kuhimiza upendo na kuwafadhili wageni;
Waebrania 13:1-2
1 Upendano wa ndugu na udumu. 2 Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.Ukiendelea kusoma unaona akisisitiza maisha ya waamini kuwa ya kumcha Bwana. Anagusia hata ndoa kuheshimiwa na watu wote (4). Anaendelea kusema watu wasipende fedha, bali waridhike na walivyo navyo, wakimshika Bwana siku zote. Mwandishi anakazia umuhimu wa kumshika Kristo, kwa sababu yeye ni yule yule, jana, leo na hata milele (8)
Somo letu asubuhi hii ni hitimisho, kukiwa na fundisho la kuchukuliana kama ndugu katika Kristo. Hapa tunakumbushwa kuwa wamoja katika Kristo Yesu, upendo ukiwa kati yetu daima. Amina.
Uwe na Jumamosi njema.
Heri Buberwa